Muswada mabadiliko ya ndoa waiva
WAZIRI wa Katiba na Sheria, Dk. Damas Ndumbaro amesema watawasilisha muswada wa mabadiliko ya ndoa ya mwaka 1971 katika bunge hili la bajeti linaloendelea .
Ndumbaro ameyasema katika Jukwaa la Wakurugenzi Wanawake waliowakilisha mashirika takribani 400 yanayotetea haki za wanawake, wasichana na watoto nchini Tanzania.
Kupitia kikao hicho Dk Ndumbaro ameeleza nia ya serikali kupitia Wizara yake kupeleka muswada wa mabadiliko ya Sheria ya Ndoa, 1971 katika Bunge hili la bajeti, ili kuweka umri wa miaka 18 kama umri wa chini wa kuolewa na kuoa.
Ndumbaro ameyasema hayo kukiwa na vuguvugu la baadhi ya viongozi wa dini kutaka umri wa kuolewa kubaki miaka 14.
Kwa mujibu wa Kifungu cha 13 na 17 vya sheria ya ndoa nchini Tanzania kinaruhusu mtoto wa kike kuolewa akiwa na umri wa miaka 14 kwa kibali cha mahakama na miaka 15 kwa ridhaa ya wazazi.
Mwaka 2019, Mahakama ya Rufaa ya Tanzania ilithibitisha uamuzi wa Mahakama Kuu katika kesi ya Rebeca Gyumi ya mwaka 2016 dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa serikali kuwa vifungu vya 13 na 17 vya Sheria ya Ndoa vinavyoruhusu mtoto kuolewa kwa idhini ya wazazi akiwa na miaka 15 na mahakama akiwa na miaka 14 ni vya kibaguzi na ni kinyume na Katiba.
Katika uamuzi huo, Mahakama Kuu iliamua kuwa Sheria ya Ndoa ipitiwe upya ili kuondoa ubaguzi na kukosekana kwa usawa kati ya umri wa chini wa ndoa kwa wavulana na wasichana.
Mahakama ilisema kuwa Kifungu cha 13 na 17 cha Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 kinakwenda kinyume na Ibara ya 12, 13 na 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ambayo inatoa haki sawa kwa wote mbele ya sheria.
Aidha, wakurugenzi kutoka Jukwaa la wanawake walitumia fursa hiyo kumhakikishia Waziri na ofisi yake ushirikiano katika kuhakikisha mchakato huo unapelekea kuwa na Sheria nzuri yenye mlengo wa kujinsia kwa ajili ya kuimarisha ulinzi kwa watoto hasa watoto wa kike.