Muswada sheria adhabu ya kifo kutua bungeni

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Pindi Chana

DSM; WAZIRI wa Katiba na Sheria Balozi Dk Pindi Chana amesema Tanzania inathamini uhai wa kila mtu, ambapo muswada wa sheria ya adhabu ya kifo utawasilishwa bunge lijalo la mwezi Novemba, 2023.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamono la kupinga adhabu ya kifo duniani leo jijini Dar es Salaam, Dk Chana amesema adhabu ya kifo ni suala la kisheria, ambalo ni kanuni ya adhabu sura ya 16, imeanzisha adhabu ya kifo kuwa adhabu zinazotolewa kwa makosa ya mauaji ya kukusudia na uhaini.

Amesema sheria hiyo ilitungwa mwaka 1945 na ilianza kufanyiwa kazi Septemba 28,1945 na baadaye umoja wa mataifa wakapitisha tamko la haki za binadamu, ambalo katika ibara ya tatu (3) linatambua haki ya kuishi na wakati sheria ya adhabu ya kifo inatungwa Tanzania ilikuwa chini ya wakoloni.

Advertisement

“Wizara imekubali kuwasilisha mapendekezo yote ya mabadiliko ya sheria kama mlivyopendekeza, mswada umewasilishwa bungeni na utajadiliwa katika Bunge linaloanza Novemba,” amesema.

Kwa upande wake Rais wa Chama cha Wanasheria nchini (TLS), Harold Sungusia amesema wanapendekeza kuwa na adhabu mbadala, ambapo badala ya kunyongwa kuwe na kifungo ambacho watakuwa wanazalisha mali kwa ajili ya familia ya waathirika.

Amependekeza kuwa serikali iwe na gereza maalum ili wafungwa wazalishe mali ambayo itawasaidia familia ya waathirika na familia yake.

“Tangu 1994 hakuna aliyetekeleza adhabu ya kunyongwa na wapo walioajiriwa, lakini hawana kazi na kuna wafungwa wapo wanatumia gharama tu hawazalishi, wafungwe kifungo cha maisha na kuwe na mfumo wa waathirika kusaidiwa,” amesema.

1 comments

Comments are closed.