Muswada sheria ya uchaguzi wagusa wadau

WADAU wa demokrasia nchini wamebainisha kuwa Muswada wa Sheria ya Uchaguzi umekuja kuziba upungufu, na sheria ikitumika vizuri ni sehemu ya upatikanaji wa Tume Huru ya Uchaguzi.

Aidha, wamepongeza fursa ya majadiliano ya muswada wa sheria hiyo ikielezwa kuwa yanatokana na weledi wa Rais Samia Suluhu Hassan akionesha ukomavu na ustahamilivu katika uongozi wake.

Kadhalika wamependekeza matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) katika chaguzi mbalimbali nchini, na kwamba muswada huo unapunguza mamlaka na madaraka ya Rais katika uteuzi wa wajumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) jambo linalotoa unafuu wa kupata wajumbe.

Wametoa maoni yao katika mkutano maalumu wa Baraza la Vyama vya Siasa unaoshirikisha wadau wa demokrasia ya vyama vingi kujadili miswada ya sheria za uchaguzi na sheria za vyama vya siasa uliomalizika jana Dar es Salaam.

Wakili Alex Mgongolwa alisema ni sheria itakayokuja kupunguza upungufu mbalimbali kwenye NEC na kubadilisha muundo na hata sifa za Mkurugenzi wa Uchaguzi. Alisema kitu muhimu ni NEC kutengeneza kanuni na kupitia kwa sheria hiyo kutasaidia kuwepo kwa uboreshaji kwa kila wakati yanapohitajika.

Mhadhiri Mwandamizi Chuo Kikuu Mzumbe, Dk Mrisho Mbegu alisema ni muswada unaobainisha dhana nzima ya kuongozwa kwa ushirikishwaji katika kupata wajumbe. Alisema ni muswada muhimu katika kupata viongozi bora, na pia kupunguza mamlaka na madaraka ya Rais katika uteuzi wa wajumbe.

“Kupitia sheria itakayopita hakuna sababu ya kuchagua tu mtu, bali kwa kushindanisha sana,” alisema Dk Mbegu na kuongeza kuwa huu ni mwanzo wa kuwa na Tume ya Uchaguzi iliyo bora zaidi kwa kuwa na wajumbe wenye sifa.

Naye Dk Hilda Lyatonga alisema sheria ya NEC itasaidia kutoa tume huru iliyokuwa inahitajika na Watanzania wengi. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, Joseph Selasini alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa mwanya kwa wadau kutoa maoni yao kuhusiana na Tume ya Uchaguzi, hivyo aliwataka wadau hao kujikita zaidi kutoa maoni yao na si kutoa kasoro zilizopita.

“Muswada huu ni muhimu kwetu hivyo tusipoteze muda kuongelea mambo mengine ila tujikiteni zaidi katika utoaji maoni,” alisema Selasini aliyewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Rombo mkoani Kilimanjaro.

Majaliwa Kyala kutoka Chama cha Sauti ya Umma aliwashukuru viongozi wa serikali kuelimisha falsafa ya Rais Samia ya R4 zake kwani zikifuatwa, wanasiasa wengi watakuwa wastahamilivu.

“Tunashukuru Rais (Samia) kwa falsafa yake (R4) ambayo tunatakiwa tuzitumie hata katika mtiririko wetu wa utoaji maoni ili sheria yetu ijayo iwe bora na kusaidia wananchi wote,” alisema Kyala.

Mwenyekiti wa Chama cha UDP, John Cheyo alitoa pendekezo kuwa falsafa ya R4 za Rais Samia zitumike katika chaguzi zote. Pia alisema sheria iseme kuwa kusiwepo na matumizi ya fedha katika uchaguzi kwa lengo la kuwepo kwa usawa kwa watu wote

Habari Zifananazo

Back to top button