Mutafungwa “ulinzi na usalama ni jukumu la kila Mwananchi”
MWANZA: WANANCHI mkoani Mwanza wametakiwa kushirikiana na Jeshi la Polisi katika suala la ulinzi na usalama ili kukomesha vitendo vya uhalifu.
Hayo yamebainishwa na kamanda wa Jeshi la polisi mkoani hapa Wilbroad Mutafungwa katika mkutano na Wananchi pamoja na viongozi wa serikali za mtaa wa Kata ya Pamba Wilaya ya Nyamagana wakati akisikiliza kero mbalimbali za kiusalama kutoka kwa Wananchi.
Kupitia mkutano huo Wananchi waliwasilisha kero na changamoto wanazokutana nazo eneo hilo ikiwemo viongozi na wazazi kushirikiana na wahalifu kwa kuwaficha baada ya kufanya uhalifu.
Akijibu kero mbalimbali kutoka kwa Wananchi hao kamanda Mutafungwa amewataka wananchi kutambua kuwa suala la ulinzi na usalama ni jukumu la kila Mwananchi kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi huku wakitoa taarifa za uhalifu na wahalifu ili hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi yao.
Mutafungwa amewataka viongozi wa serikali za mitaa kutokumbatia vitendo vya uhalifu.