MHALIFU wa makosa ya ubakaji na mauaji raia wa Afrika Kusini aliyetoroka gerezani na kukamatwa jijini Arusha wiki iliyopita, amesafirishwa kwa ndege jana kurudishwa nchini humo.
Thabo Bester alitoroka gerezani Mei mwaka jana kwa kutunga taarifa za kifo chake katika ajali ya moto na kuweka mwili bandia katika chumba chake cha gereza.
Alikamatwa pamoja na mpenzi wake ambaye ni daktari maarufu, Nandipha Magudumana.
Wawili hao waliwasili kwa ndege kwenye kiwanja cha ndege kilichopo viungani mwa mji wa kibiashara wa Johannesburg.
Aidha, baba yake mzazi Nandipha naye amefunguliwa mashtaka kwa kumsaidia mtoto wake kutoroka gerezani.
Bester amekuwa akitafutwa baada ya kubainika alighushi kifo chake kutokana na ripoti iliyotoka mwezi uliopita ikionesha mtu aliyedhaniwa kuwa ni yeye hakuwa yeye.
Mbali ya baba yake Nandipha, Zolile Sekeleni, pia Msimamizi wa gereza Senohe Matsoara amefunguliwa mashtaka ya mauaji, uchomaji moto na kusaidia kutoroka kwa mfungwa huyo.
Wawili hao walisimamishwa kizimbani Bloemfontein mapema wiki hii na hakutakiwa kujibu chochote. Kesi hiyo iliahirishwa hadi Jumatatu ijayo.
Kwa mujibu wa Polisi nchini humo, Bester baada ya kuwasili nchini humo amepelekwa katika gereza lenye ulinzi mkali katika mji mkuu Pretoria, huku mpenzi wake akifikishwa mahakamani huko Bloemfontein.
Atashtakiwa kwa makosa ya mauaji, ulaghai na kumsaidia Bester, wakati Bester akitarajiwa kukabiliana na makosa mengine mapya baada ya kutoroka.
Bester anajulikana kama ‘Mbakaji wa Facebook’ kwa kutumia mtandao huo wa kijamii kuwarubuni waathirika wake. Alipatikana na hatia mwaka 2012 kwa kumbaka na kumuua mpenzi wake mwanamitindo, Nomfundo Tyhulu.
Mwaka mmoja baadaye, alipatikana na hatia ya kubaka na kuwaibia wanawake wengine wawili.
Kutoroka kwa Bester kulizua hasira nchini Afrika Kusini, ambayo ina mojawapo ya viwango vya juu zaidi vya unyanyasaji wa kingono duniani.
Comments are closed.