Muuguzi mbaroni kwa kumbaka mjamzito
MUUGUZI wa daraja la pili katika Hospitali ya Sikonge mkoani Tabora, Rayson Duwe ametiwa mbaroni na jeshi la polisi kwa kumbaka binti mjamzito ambaye alilazwa katika hospitali hiyo akisumbuliwa na ugonjwa wa malaria na UTI.
Tukio hilo limetokea Juni 9, 2023 saa mbili usiku ambapo kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora ACP Richard Abwao amedai kuwa siku ya tukio muuguzi huyo aliingia kazini akiwa amelewa.
“Kitendo hiki si cha kiungwana, na muuguzi huyu alitenda kosa hili wakati alipopangiwa zamu ya usiku ya kuhudumia wagonjwa wa nje (OPD).”Amesema Kamanda Abwao
Amesema, muuguzi huo alitoka na kwenda chumba cha wagonjwa wa ndani na kumbaka binti huyo mwenye ujauzito wa karibu kujifungua.
Muuguzi huyo alikutwa akiwa na bomba la sindano pamoja na dawa za usingizi huku taarifa ya kitabibu zikithibitisha kuwa alimwingilia mgonjwa huyo.
Mtuhumiwa huyo amefikishwa mahakamani mapema hii leo June 13, 2023 kujibu tuhuma zinazo mkabili baada ya upelelezi kukamilika.
Nae, Mkuu wa Wilaya ya Sikonge Simon Chacha amesema baada ya tukio hilo Serikali imechukua hatua za kinidhamu kwa kumsimamisha kazi Muuguzi.