Mv Mwanza Hapa Kazi kuzinduliwa Jumapili

MELI ya Mv Mwanza Hapa Kazi itashushwa katika maji Jumapili wiki hii kwa ajili ya matengenezo ya mwisho.

Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL), Eric Hamissi, amesema ujenzi wake umefikia asilimia 82 na kazi zote kubwa zinazohusisha hasa ufungaji wa mashine mbalimbali zimeshakamilika.

Asilimia 18 iliyobaki itahusisha pamoja na mambo mengine,  ufungaji wa mitambo ya kuendeshea meli, viti, vitanda, dari, viyoyozi na kupaka rangi.

“Kwa ujumla umbo lote la meli limeshakamilika. Lengo kuu la kushushwa katika maji ni kuangalia uimara wa kazi iliyokwishafanyika, ikiwemo kuchunguza kama kuna sehemu inavujisha,” amesema.

Sambamba na hilo, Hamissi amepongeza jitihada za serikali ya Awamu ya Sita katika kuongeza kasi ya ujenzi wa meli hiyo, akasema:

“Wakati Rais Samia Suluhu Hassan anaingia madarakani ujenzi ulikua asilimia 45. Kiasi kikubwa cha fedha kimelipwa ndani ya hii miezi 22 na kufanikisha kufikia hatua tuliopo sasa, ” amesema.

 

Mv Mwanza inatarajia kukabidhiwa rasmi kwa MSCL mapema mwezi Agosti mwaka huu, ili kupangiwa ratiba ya safari katika Ziwa Victoria.

Safari zake zinatarajiwa kuwa katika bandari zote kubwa katika ziwa Victoria, ikiwemo Jinja na Port Bell (Uganda) pamoja na Kisumu (Kenya).

 

Habari Zifananazo

Back to top button