Mv Mwanza kuongeza tija SGR

Sh bilioni 117 zatengwa miradi Ziwa Victoria, Nyasa, Tanganyika

WIZARA ya Ujenzi na Uchukuzi imesema serikali iliamua kujenga meli kubwa katika Ziwa Victoria ili kukidhi mahitaji ya soko yanayotarajiwa kuongezeka baada ya kukamilika ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza.

Naibu Waziri wa wizara hiyo, Atupele Mwakibete alisema Mwanza jana kuwa tija ya reli hiyo itaongezeka kama kutakuwa na meli kubwa kwa ajili ya kutumia masoko kwenye nchi jirani.

Mwakibete alisema hayo wakati wa hafla ya kuitoa meli ya Mv Mwanza ‘Hapa kazi tu’ na kuiingiza majini kuashiria kukamilika kwa ujenzi wa umbo la chombo hicho cha kisasa ambacho ujenzi wake umefikia asilimia 82.

Advertisement

“Kujengwa kwa meli hii kutasaidia kufungua masoko mapya ndani na nje ya nchi kwa kuanzisha safari mpya zitakazosaidia kurahisisha shughuli za kibiashara, kikazi, utalii na safari binafsi kwenye maeneo mengi zaidi kuliko ilivyo sasa”alisema.

Mwakibete alisema ujenzi wa meli hiyo ukikamilika itaboresha usafiri kwenye maziwa makuu kwa kutoa huduma katika bandari za Kisumu nchini Kenya, Kemondo na Bukoba mkoani Kagera, Jinja na Port Bell nchini Uganda, Musoma mkoani Mara na Mwanza.

Aliaigiza Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) iziboreshe bandari katika Ziwa Victoria ili meli hiyo itie nanga bila tatizo na ifanye kazi kwa ufanisi.

Mwakibete alisema Rais Dk Samia Suluhu Hassan ameielekeza Wizara ya Ujenzi na uchukuzi katika bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023 katika ziwa Tanganyika kutengeneza meli kubwa tatu za abiria na mizigo.

Alisema meli ya kwanza itakuwa inabeba abiria 600 na tani 400 za mizigo, meli ya pili itakuwa inabeba tani 3,500 na  chelezo kubwa yenye uwezo wa kubeba tani 5,000 lakini pia katika ziwa Victoria itajengwa meli nyingine mpya ya mizigo yenye kubeba uzito wa tani nyingine za mizigo 3,500.

Awali Mkurugenzi wa Kampuni ya Huduma za Meli (MSC), Eric Hamissi alisema meli hiyo yenye urefu wa mita 92.6 na upana wa mita 17 ni kubwa zaidi katika maziwa makuu yote Afrika.

Hamissi alisema meli hiyo yenye ghorofa tano itakuwa na lifti yenye uwezo wa kubeba watu 20 kwa wakati mmoja ikiwa na uwezo wa kubeba abiria 1,200, tani 400 za mizigo na magari zaidi ya 20 kwa wakati mmoja.

Alisema hadi itakapokamilika itakuwa na uzito wa tani 3,500 ikiwa na mgahawa, zahanati na ukumbi wa muziki unaowezesha maonesho ya bendi mubashara.

Hamissi alisema mradi huo unatekelezwa kwa gharama ya shilingi bilioni 109.15 na inajengwa na Watanzania zaidi ya 300 wenye umri wa miaka 21-35.

Alisema meli hiyo itakuwa na madaraja sita vikiwamo vyumba viwili vya viongozi, vyumba vinne vya watu mashuhuri, daraja la kwanza abiria 60, daraja la biashara abiria 100, daraja la pili abiria 200 na daraja la kawaida abiria 834.

Hamissi alisema miezi minne hadi mitano kuanzia sasa mkandarasi ataitumia kufunga vifaa vya ndani vikiwamo vitanda, viti, viyoyozi, vyoo na kupaka rangi na urembo mwingine.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *