MELI ya Mv Mwanza ‘Hapa kazi’ ni meli kubwa kuliko zote zilizowahi kuelea katika maziwa ya Victoria, Tanganyika na Nyasa hapa nchini na inatarajiwa kuingia rasmi majini Oktoba mwaka huu.
Hayo yameelezwa leo Septemba 5, 2022 na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Huduma za Meli( MSCL), Eric Hamissi, wakati akitoa taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa meli hiyo kwa Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Abdulrahman Kinana, katika ziara ya kukagua miradi inayotekelezwa na serikali pamoja na kukagua uhai wa chama.
Amesema ujenzi huo umefikia asilimia 71 na unagharimu Sh bilioni 89 na itakuwa na uwezo wa kusafiri kwa saa saba tu kutoka Mwanza kwenda Bukoba, ikitofautiana na meli zilizopo kwa sasa ambazo zinatumia saa saba hadi 12 kwenda Bukoba.
Alisema pia itakuwa inafanya safari katika nchi za Uganda katika bandari za Portbell na Jinja na bandari ya Kisumu nchini Kenya na Kemondo kwa Tanzania na Bukoba.
“Tunafikiria pia kuipeleka Bandari ya Musoma mkoani Mara kutokana na soko litakavyokuwa, kwa sababu ina uwezo mkubwa wa kubeba mizigo, ”alisema
Kwa upande wake, Kinana ameupongeza uongozi wa Mkoa wa Mwanza kupitia Kampuni hiyo ya Huduma za Meli (MSCL) kwa hatua nzuri waliyofikia kwa ajili ya ujenzi wa meli hiyo mpya ya Mv Mwanza.
“Nawapongeza nyote kwa kazi nzuri iliyofanyika”, alisema Kinana wakati alipotembelea meli hiyo katika Bandari ya Mwanza Kusini, akiongozana na viongozi mbalimbali wa CCM akiwemo Katibu wa Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka.