Mvua yaleta changamoto uchaguzi Kigoma

UPIGAJI kura katika uchaguzi mdogo wa udiwani kata ya Kasingirima Manispaa ya Kigoma Ujiji umeendelea, huku ikielezwa hali ya amani na usalama ikitawala, licha ya kuwepo idadi ndogo ya watu wanaojitokeza kupiga kura kulikosababishwa na mvua iliyonyesha.

Msimamizi wa uchaguzi huo,Mwantumu Mgonja akizungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi ya Mtendaji Kata ya Kasingirima, ambapo shughuli ya kuhesabu na kufanya majumlisho ya kura itafanyika, alisema kuwa hadi sasa hakuna changamoto yeyote iliyojitokeza na kwamba wanaamini uchaguzi utaisha salama.

Mgonja alisema kuwa vyama 12 vimeweka wagombea kwenye uchaguzi huo, huku kukiwa na jumla ya watu 1964 wanaotarajia kupiga kura katika vituo sita vilivyoteuliwa.

Mgombea wa CCM katika uchaguzi huo,Mlekwa Kigeni alisema kuwa hadi sasa hajasikia kuwepo kwa changamoto kwenye uchaguzi na anaamini kwamba utaisha vizuri, licha ya idadi ndogo iliyojitokeza asubuhi kwa sababu ya mvua kubwa, lakini kufikia mchana huu idadi ya watu imeanza kuongezeka.

Kwa upande wake Katibu Mipango na  Uchaguzi ACT Mkoa Kigoma,Issa Hussein alisema kuwa uchaguzi unaenda vizuri tangu ulipoanza lakini zipo changamoto ndogondogo.

Habari Zifananazo

Back to top button