Mvua yasababisha kifo Katavi

ELIZABETH Fabiano(32) mkazi wa Mtaa wa Shanwe Manispaa ya Mpanda Mkoa wa Katavi,  amefariki baada ya kuangukiwa na nyumba kutokana na mvua kubwa kunyesha iliyoambatana na upepo mkali alipokuwa amelala usiku.

Akizungumzia tukio hilo mama mzazi wa marehemu, Khadija Eneliko (60) ambaye ni mjane, amesema mtoto wake Elizabeth amekufa usiku wa kuamkia Jumapili Aprili 16, 2023 walipokuwa wamelala kwenye nyumba hiyo.

“Tulipokuwa tumelala kidogo usiku tukasikia mvua inanyesha na baada ya muda kidogo tukasikia ukuta wa nyumba unaanguka kwa nguvu na hapo mwanangu ukuta ukamdondokea sehemu ya mgongo na maeneo mengine ya mwili, ” amesema Khadija.

Ameeleza kuwa baada ya hapo aliomba msaada kwa majirani na walimpeleka hospitali ya Manispaa ya Mpanda, lakini akiwa anapatiwa matibabu alifariki.

Waombolezaji wakiwa katika msiba wa Elizabeth Fabiano aliyefariki kwa kuangukiwa na nyumba Mtaa wa Shanwe.(Picha zote na Swaum Katambo).

 

Kwa upande wake Mjumbe wa serikali ya Mtaa wa Shanwe, Lazaro Kakamba amethibitisha kutokea kwa tukio hilo katika mtaa wake na kusema kuwa wamesikitishwa na tukio hilo kwa kuwa waliishi vizuri na marehemu Elizabeth.

Kakamba ameiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kuwasaidia wazee hasa wasiojiweza kwa kuwaingiza katika Mfuko wa Maendeleo Jamii (TASAF), ili waweze kujikwamua kiuchumi kutokana na mama mzazi wa marehemu kubaki peke yake katika nyumba hiyo iliyobomoka, ambapo tegemezi lake kubwa lilikuwa ni binti huyo aliyefariki.

Kwa upande wao baadhi ya majirani wameiomba Serikali kuona namna ya kumsaidia mama mzazi wa marehemu, Khadija Eneliko ili aweze kupata mahali salama pa kuishi.

Khadija Eneriko Mkazi wa Mtaa wa Shanwe aliyepoteza mtoto wake kwa kuangukiwa na nyumba.

“Tunaomba serikali iweze kuangalia uwezekano wa kumjengea nyumba nyingine bibi huyu, kwani hapa alipo mazingira siyo salama nyumba bado inaonekana kuwa na nyufa, ” amesema Rehema Juma mkazi wa Mtaa wa Shanwe.

 

Habari Zifananazo

Back to top button