Mvua za El-Nino zasababisha vifo 155
DODOMA: WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema zaidi ya Kaya 51,000 na watu 200,000 waliathirika na Mvua kubwa za El-nino zilizoambatana na upepo mkali, mafuriko na maporomoko ya udongo katika maeneo mbalimbali Nchini ambapo watu 155 walipoteza maisha; na watu wapatao 236 walijeruhiwa na nyumba zaidi ya 10,000 ziliathirika kwa viwango tofauti.
Majaliwa ametoa taarifa hiyo Aprili 25, 2024 Bungeni Jijini Dodoma wakati akitoa tamko la Serikali kuhusu matukio ya hali ya hewa nchini ambapo amesema maeneo mengine yaliyoathirika ni pamoja na miundombinu ya shule, zahanati, nyumba za ibada, barabara, madaraja, mifugo na mashamba yenye mazao mbalimbali.
“Baadhi ya maeneo yaliyoathirika niliyatembelea na kujionea hali halisi. Hivi karibuni, mimi pamoja na Mawaziri nane wa Kisekta tulitembelea maeneo ya Mlimba, Ifakara na Malinyi (Morogoro) na Rufiji (Pwani). Nilitumia fursa hiyo kuwasilisha salamu za pole za Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuwajulisha kuhusu misaada inayotolewa na Serikali ya Awamu ya Sita”
“kipekee niwashukuru wadau mbalimbali nchini ambao wamekuwa mstari wa mbele kuungana na Serikali kuwasaidia Watanzania wenzetu waliopatwa na majanga. Nitumie fursa hii kuendelea kuwasihi Watanzania wenzangu kuungana na Serikali kuwasaidia wananchi wenzetu wanaopatwa na majanga mbalimbali”. Majaliwa
Baadhi ya maeneo yaliyoathirika nchini ni pamoja na Rufiji na Kibiti (Pwani); Malinyi, Mlimba, Kilosa, Manispaa ya Morogoro, na Ifakara (Morogoro); Ilala, Kinondoni, Ubungo, Kigamboni na Temeke (Dar es Salaam); Same, Hai na Moshi (Kilimanjaro); Mbarali, Kyela na Halmashauri ya Jiji la Mbeya (Mbeya); Manispaa ya Kigoma Ujiji na Kakonko (Kigoma); Iringa Vijijini (Iringa); Manispaa ya Tabora (Tabora); Bahi (Dodoma); Lindi Manispaa, Kilwa, Liwale, na Nachingwea (Lindi), Masasi (Mtwara) na Arusha Jiji, Monduli na Karatu (Arusha).
Maeneo mengine ni (Muleba, Bukoba Manispaa (Kagera); Manispaa ya Shinyanga (Shinyanga); Geita Mji, Nyangh’wale na Chato (Geita); Mbozi na Momba (Songwe); Nkasi, Sumbawanga na Kalambo (Rukwa); Hanang’ (Manyara).