Mvua zaanza, TMA yatoa hadhari

Mvua yawatenga wananchi wa Kata ya Maboga na wengine

MAMLAKA ya Hali ya Hewa (TMA) imehadharisha uwezekano wa mvua kubwa kujaza maji kwenye makazi ya watu katika mikoa minne nchini kuanzia leo  hadi Alhamisi wiki hii.

Kupitia ukurasa wake katika mtandao wa kijamii wa twitter, TMA imetoa angalizo la mvua kubwa leo katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani ikihusisha visiwa vya Mafia, Lindi na Mtwara.

TMA ilihadharisha kuwa mvua hizo zinaweza kujaza maji kwenye makazi na kuathiri shughuli za kiuchumi.

Advertisement

Mvua zilizonyesha jana kwenye maeneo kadhaa ya Dar es Salaam zilisababisha adha kwa wananchi wakiwamo waliokuwa na magari kushindwa kuendelea na safari.

Barabara kadhaa jijini Dar es Salaam ikiwamo ya Nyerere eneo la Kamata na Bagamoyo zilijaa maji na kukwamisha usafiri.

Tahadhari pia imetolewa ya mvua kubwa keshokutwa katika maeneo mengi ya mikoa ya Mtwara na Lindi na zinaweza kujaza maji kwenye baadhi ya makazi na kuathiri shughuli za kiuchumi.

Hivi karibuni Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ilitoa ushauri kwa mamlaka za mikoa minne zichukue tahadhari kukabili mvua nyingi za masika zilizotarajia kuanza wiki ya pili na ya tatu ya mwezi huu.

Alitaja mikoa hiyo kuwa ni Dar es Salaam, Pwani, Morogoro na visiwa vya Unguja na Mafia ambapo katika mvua za masika zitapata mvua za wastani hadi juu ya wastani.

Aidha TMA ilisema katika simu wa mvua za masika mwaka huu takribani mikoa 11, zinatarajiwa kunyesha mvua za wastani hadi chini ya wastani.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Ladislaus Chang’a alisema mvua za masika ni mahsusi kwa maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki, pwani ya kaskazini na kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma.

Chang’a alisema kutokana na mifumo ya hali ya hewa inayotarajiwa katika kipindi cha msimu, mvua za wastani hadi juu ya wastani zitanyesha katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani katika visiwa vya Mafia, Kaskazini mwa Mkoa wa Morogoro na kisiwa cha Unguja.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *