Mvua zakimbiza samaki

SAMAKI aina ya dagaa mchele na saladini wameadimika katika soko la Kimataifa la Samaki Feri mkoani Dar es Salaam na kusababisha kupaa kwa bei ya kitoweo hicho.

Ofisa Uvuvi wa soko hilo, Abeid Shamte akizungumza alisema hali hiyo inasababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa baharini.

“Kama unakumbuka ulivyokuja Septemba 2023 nilikueleza sababu za kitaalamu za ukosekanaji wa samaki na kukuahidi endapo hakutakuwa na mabadiliko ya tabianchi huenda samaki wakaongezeka,” amesema Shamte na kuongeza kuwa pamoja na kuongezeka katikati ya mwezi Oktoba mwanzoni mwa Novemba hali imebadilika

Shamte amesema lakini uadimikaji wa awali na wa sasa una tofauti yake, kwa sababu mwezi Mei hadi Septemba ni msimu wa baridi kwa ukanda wa mwambao wa Pwani na hakuna mvua kali na ngurumo lakini safari hii kuna mvua kubwa zilizoanza Novemba, 2023.

“Samaki ana tabia moja bahari inapochafuka hususani mvua zinazosababisha mito kufurika na kuelekea baharini kunakosekana utulivu na hivyo samaki hutafuta maficho zaidi kwa sababu maji yaingiayo baharini huja na takataka, udongo na kila aina ya uchafu hivyo husombwa na maji kuelekea umbali mrefu ambapo hata wavuvi wakati mwingine hawezi kufika,” amesema.

Wafanyabiashara wakizungumza na HabariLEO sokoni hapo ili kubaini bei ya samaki kwa ndoo ya lita 20 walisema bei ya dagaa mchele imetoka Sh 30,000 hadi Sh 100,000 wakati wiki mbili zilizopita ndoo ya saladini ilikuwa Sh 40,000 na sasa imefika Sh 100,000.

Kutokana na hali hiyo samaki kwa bei ya rejareja mitaani haijapanda isipokuwa vipimo vya ujazo vimekuwa finyu mno kwa maana ya ukadiriaji wa mafungu bado fungu ni Sh 1,000 lakini halina ukubwa kama ule wa kipindi samaki wanapopatikana kwa wingi.

Je umejisajili #MwangwiwaUkarimu #EchoesofKindness

Habari Zifananazo

6 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button