‘Mwagilia moyo’ kwa lishe bora kuepuka NCDs

RIPOTI ya Shirika la Afya Duniani (WHO) inaonesha kuwa vifo milioni saba vitokanavyo na magonjwa yasiyoambukiza vinaweza kuzuiwa ifikapo mwaka 2030, ikiwa nchi zenye kipato cha chini na cha kati zitawekeza katika kuzuia na kutibu magonjwa hayo.

Magonjwa yasiyo ya kuambukiza (NCDs) ni pamoja na ugonjwa wa moyo, kisukari, saratani na magonjwa ya mfumo wa upumuaji ambayo yamekuwa yakisababisha vifo saba kati ya vifo 10 duniani.

Magonjwa yasiyo ya kuambukiza husababishwa na mambo mbalimbali ikiwamo matumizi ya tumbaku na pombe, mtindo mbaya wa maisha, ulaji usiofaa na kutofanya mazoezi maarufu kama tabia bwete.

Ukweli ni kwamba asilimia 85 ya vifo vya mapema kati ya umri wa miaka 30 hadi 69 vinatokana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza, hutokea katika nchi zenye kipato cha chini na kuzifanya kuwa na mzigo mkubwa kiafya, kijamii na kiuchumi.

Upo msemo ‘mwagilia moyo’ uliopata umaarufu katika mitandao ya kijamii ukimaanisha matumizi ya unywaji wa pombe kwa lengo la kufurahisha mwili.

Hili jambo si la kufanyiwa mzaha kwa sababu matumizi ya pombe ni njia mojawapo inayoongeza magonjwa yasiyoambukiza kama vile kisukari na magonjwa ya moyo.

Ieleweke kuwa matumizi ya pombe kupita kiasi ni hatari kwa afya, hivyo njia mbadala ni kuongeza matumizi ya maji ili kuboresha afya na kuepukana na magonjwa.

Lakini pia ni wakati wa kuacha tabia bwete kwa kuhakikisha mwili unashughulishwa ama kwa kufanya mazoezi au kazi mbalimbali za nyumbani.

Katika kitabu kilichoandaliwa na Wizara ya Afya ambacho kinapatikana kwenye mtandao, kinaelezea namna bora ya kuepuka magonjwa hayo ikiwemo njia za kukabiliana na msongo wa mawazo.

Kama ambavyo matumizi ya sayansi na teknolojia yameongezeka nchini, ni wakati wa kutumia mitandao vizuri kwa kupakua kitabu hicho ili kujisomea na kujipatia elimu juu ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza.

Nia ya serikali ni kudhibiti ukubwa wa magonjwa haya hivyo ni lazima kuonesha jitihada kwa kusoma vitabu na kupata elimu mbalimbali jinsi ya kuepuka magonjwa hayo.

Kila mtu akichukua hatua kwa kuzingatia lishe inayofaa kwa kula chakula kutoka katika makundi matano ya chakula ikiwamo vyakula vya wanga, protini, mboga za majani, mbogamboga na mafuta, chumvi na sukari kiasi, atakuwa katika nafasi nzuri ya kuepuka magonjwa yasiyo ya kuambukiza.

Pia endapo jamii itaepuka matumizi ya pombe kupindukia na tumbaku, naamini kwa kiasi kikubwa magonjwa haya yatapungua ifikapo mwaka 2030 kama serikali ilivyojiwekea malengo yake.

Magonjwa yasiyo ya kuambukiza husababisha athari kubwa kiuchumi kwa ngazi ya familia na taifa kwa ujumla kwa sababu unapopatwa na ugonjwa mmoja wapo kati ya magonjwa niliyoyaeleza, utapaswa kutumia gharama kubwa za matibabu.

Endapo tutachukua hatua stahiki mapema, fedha zingetumika kuboresha sekta za afya, elimu, ujenzi, uchukuzi, mawasiliano na nyingine.

Jambo la msingi na la muhimu kuzingatia ni kuhakikisha unapima afya yako mara kwa mara. Hatua hii inasaidia, endapo mtu anagundulika kuwa na ugonjwa, inampa nafasi ya kuanza tiba mapema hivyo kuongeza uwezekano wa kupona.

Wakati ni huu wa kuweka nguvu za pamoja kati ya jamii na serikali katika kudhibiti magonjwa yasiyo ya kuambukiza.

Vilevile jamii hususani vijana wanapaswa kupunguza matumizi ya vilevi kwa kigezo cha kumwagilia moyo. Badala yake, wamwagilie mwili wote kwa kuzingatia mfumo wa maisha unaofaa ikiwamo kupata lishe bora na kufanya mazoezi.

 

 

 

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button