Mwakitalima afafanua hali kwa wanaopoteza choo

Kilele wiki ya usafi

MTU mmoja ambaye hana choo hupoteza takribani saa 58 kwa mwaka kutafuta muda wa kujisitiri.

Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Afya, Mazingira kutoka Wizara ya Afya Anyitike Mwakitalima amesema hayo wakati  wa kilele Cha wiki ya usafi wa Mazingira na mashlndano ya usafi mwaka 2022, Iliyofanyika Jijini hapa.

Alisema kuwa sawa mtu ambaye hana choo hupoteza takribani saa 58 kwa mwaka kutafuta mahali pa kujistiri.

Advertisement

Pia alisema kiini cha magonjwa ambayo yanamkabili mwanadamu yanayokana na mwingiliano baina yake na mazingira yanayomzunguka.

Alisema kuwa dhima ya Wizara ni kuhakikisha kuwa afya bora kwa Kila mwananchi. “Hatuna chaguo lingine zaidi ya kuwekeza nguvu na raslimali za kutosha kweye eneo la kinga hususan afya Mazingira,” alisema.

Alisema kuwa ripoti ya Benki ya Dunia inaeleza kwamba tunapowekeza shilingi moja kwenye usafi wa mazingira tunaokoa shilingi tisa ambazo zingetumika kwa namna yoyote kugharamia madhara yoyote ambayo yangetokana na uchafu ikiwemo gharama za kutibu magonjwa, muda wa uzalishaji unapotea , vifo vya mapema na athari nyingine nyingi.

Kwa upande wake Naibu Katibu mkuu Wizara ya Afya, Dk Seif Shekalaghe alisema kuwa Tanzania, uwepo wa vyoo bora kwa upande wa kaya umeongezeka sana katika kipindi cha miaka10 iliyopita. Mathalani, vyoo bora katika ngazi ya kaya umeongezeka kutoka asilimia 19.5 mwaka 2012 hadi kufikia asilimia 72.6 mwaka 2022.

Kaya zisizokuwa na vyoo kabisa zimepungua kutoka asilimia 20.5 hadi kufikia asilimia 1.4 sasa. Aidha, ujenzi wa vyoo bora pamoja na uwepo wa huduma za maji safi na salama umeongezeka katika taasisi.

“Kwa mfano shule za msingi na vituo vya kutolea huduma za afya. Ndani ya kipindi cha miaka mitatu iliyopita takriban shule za msingi 2,500 zimejengewa vyoo bora,” alisema. Aidha, vituo vya kutolea huduma za Afya vipatavyo 1,500 vimeboreshewa huduma ya maji, vyoo na sehemu za kunawa mikono.