Mwamba umeanguka, kwaheri Mfalme wa soka Pele

Samia atuma salamu za rambirambi kifo cha Pele

MWAMBA umeanguka! Kwaheri Mfalme wa Soka,  Edson Arantes do  Nascimento almaarufu, Pele.Mfalme wa soka Pele  hatunae tena duniani. Amefariki katika Hospitali ya Albert Einstein jijini Sao Paulo, Brazil Desemba 29, 2022 akiwa na umri wa miaka 82.

Mcheza kandanda aliyezaliwa katika familia duni huko Brazil ametangulia mbele ya haki, Mfalme wa soka Pele, hakuna aliyetilia shaka juu ya ufundi wake katika kusakata kabumbu.

Pele, atabaki katika kumbukumbu ya ulimwengu wa soka kama alama na nguzo muhimu ya mafanikio ya mchezo huo.

Advertisement

Naam! Mfalme wa soka Pele – mshumaa katika upepo, umezimika ghafla,  daima tutakuenzi sio tu kwenye mchezo wa mpira wa miguu bali hata katika siasa, Pele alieneza ujumbe wa amani, umoja, upendo, haki , usawa kwa watu wote.

Wakati wa uhai wake hakuwa mtu wa visasi, chuki wala ubaguzi, daima alikuwa mtu wa watu.

Simanzi, kubwa kwa familia yake,  ulimwengu  wa soka, kwa hakika Brazil imeondokewa.

Pele kama nilivyoeleza awali, amezaliwa katika familia ya kimaskini,  kipaji chake kilianza kuonekana tangu utotoni mwake.

Mwalimu wa soka, De Brinto  wa timu ya Santos atabaki katika shajara ya wanasoka wengi kwa kuibua kipaji cha Pele kiasi kwa kumtoa katika timu ya wachezaji wadogo ya Bauru Athletic na kumpeleka katika timu kubwa kwa majaribio ya Santos F.C.

Kwa sababu ya uwezo na uhodari wake katika kusakata kabumbu, Pele alifaulu majaribio na kuchukuliwa katika timu ya Santos.

Akiwa na umri wa miaka 16, Pele katika kipindi kifupi sana alianza kuonesha uwezo na ujuzi katika kucheza soka ambapo akiwa na umri wa miaka 17 alichaguliwa katika timu ya Taifa ya Brazil.

Akiwa katika timu ya Taifa, Pele alionesha uwezo mkubwa na kwa mara ya kwanza kucheza fainali za Kombe la Dunia mwaka 1958, ambapo alicheza kwa ufundi mkubwa akisaidia timu ya Taifa lake kutwaa ubingwa kwa kuwafunga wenyeji wa mashindano hayo, timu ya Taifa ya Brazil.

Katika fainali hizo zilizofanyika Sweden mwaka 1958, Pele alifunga magoli bora zaidi katika hatua ya  nusu fainali na fainali ikiwa ni fainali yake ya mwanzo kabisa, huku mashabiki wa soka wakianza kuona uwezo wake katika soka akiwa kijana mdogo kabisa.

Pele amecheza fainali za Kombe la Dunia za mwaka 1958, 1962 na mwaka 1970 ambapo katika fainali hizo, Pele amefunga magoli 12 katika michezo 14 ya Kombe la Dunia.

Mfalme wa soka amecheza jumla ya mechi 694 za klabu yake huku akifunga magoli 650, ambapo katika timu ya Taifa ya Brazil, mfalme huyo wa soka amecheza mechi 92 na kuifungia timu ya Taifa jumla ya magoli 77.

Pele amezaliwa Oktoba 23, 1940, Baba yake mzazi Joao Ramos do Nascimento naye alikuwa mchezaji mpira,ingawa hakuwa maarufu kama mwanae Pele.

Kwa kuwa familia yake ilikuwa ni maskini, Pele hakuweza kupata kununuliwa mpira wa kuchezea, alilazimika kuchukua soksi na kuifuma kama mpira kisha kuanza kuchezea.

Maisha yake Pele yalikuwa magumu, licha ya kuwa na umri mdogo alijiingiza katika shughuli za kujitafutia kipato, lakini kwa kuwa kipaji chake ni soka, Pele alijiegemeza katika mchezo huo.

Pele hakubahatisha kucheza soka,  anajua hasa kucheza mchezo huo.

Pele amestaafu soka mwaka 1977, ambapo timu yake ya mwisho kucheza ni New York Cosmos.

Kwaheri Mfalme wa Soka,Pele Mwamba umeanguka!

*Makala haya yameandikwa kutoka vyanzo mbalimbali kweny mtandao.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *