Mwanafunzi achangisha Sh Mil 100 kusaidia wenye usonji

KIASI cha Sh milioni milioni 100 kimechangishwa kusaidia kutekeleza huduma ya mazoezi tiba kwa wanafunzi wa kituo cha Msimbazi Mseto Ilala, Dar  es Salaam kitengo cha Usonji.

Fedha hizo zimechangiwa na mwanafunzi wa kidato cha nne wa International School of Tanganyika (IST), Madeleine Kimario kwa ajili ya Mfuko wa taasisi ya Lukiza Autism kutekeleza huduma hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari, wakati wa kukabidhi hundi hiyo,  Madeleine Kimario amesema kuwa, mradi huo na ushirikiano wake na Lukiza  Autism Foundation, utajumuisha upatikanaji wa mazoezi tiba kazi na usafiri wa kwenda na kutoka shule.

“Chakula kwa ajili ya kuhakikisha watoto wanapata lishe bora shuleni, vifaa vya mazoezi tiba na ukarabati wa madarasa ya kutolea huduma za mazoezi tiba,” amesema.

Kwa upande wake mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa Lukiza Autism Foundation, Hilda Nkabe ameelezea kuwa kuelimisha jamii kuhusu usonji na kusaidia gharama za mazoezi tiba kwa watoto wenye usonji ni moja ya malengo ya Lukiza Autism Foundation.

Amesema kuwa malengo haya yameenda sambamba na mradi wa Madeleine Kimario, aliouchagua kufanya kama sehemu ya masomo yake ya kidato cha nne.

“Mradi huu umezinduliwa Januari 18, 2023 na utaanza na ukarabati wa madarasa ya mazoezi tiba na ununuzi wa vifaa tiba na kufuatiwa na utoaji wa huduma ya mazoezi ifikapo mwezi wa pili mwaka huu.

“Gharama za mradi huu kwa mwaka huu wa kwanza ni takriban Sh Millioni 150, hivyo Hilda Nkabe

anawasihi na kuwakaribisha wafadhili wengine na wadau  kuendelea kuunga mkono juhudi za Lukiza, ili kukamilisha mradi huu,” amesema.

Pia ameongeza kuwa lengo la Lukiza Autism ni kuweza kutoa huduma endelevu kwa wanafunzi wote 45 waliopo kituoni hapo kwa sasa.

Naye Ofisa Elimu Maalum Jiji la Ilala, Swalehe Msechu kwa niaba ya Shule ya Msingi ya Msimbazi Mseto kitengo cha usonji , alimshukuru Madeleine Kimario na Lukiza Autism kwa hatua hiyo.

Habari Zifananazo

Back to top button