Mwanahabari akemea matukio ukatili kwa watoto

MWANAHABARI mtetezi wa watoto na wanawake, Dk Tumaini Msowoya amelaani matukio ya kikatili dhidi ya watoto likiwemo la hivi karibuni mjini Iringa lililomuhusisha baba kumnyonga mwanaye huku akijirekodi video.

Baba huyo, Goodluck Mgovano (35) mkazi wa mtaa wa Kota kata ya Mlandege mjini Iringa anatuhumiwa kumuua mtoto wake wa miaka minne kwa kumnyonga kwa kamba ya viatu huku akirekodi tukio hilo la kinyama kwa simu yake ya mkononi na kisha kuacha ujumbe mfupi wa maandishi kuelezea chanzo cha mauaji hayo na wapi angetamani mwili wa mtoto huyo uzikwe.

Dk Msowoya ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Siasa Mkoa wa Iringa alisema; “Watoto ni waathirika wasio na hatia wa matukio haya ya ukatili hivyo wanapaswa kulindwa na kulelewa kwa upendo na heshima.”

Advertisement

Akizungumza na mamia ya waumini wa Kanisa Katoliki, Kigango cha Mbigili wakati akimuwakilisha Mbunge wa Jimbo la Kilolo, Justine Nyamoga kwenye uzinduzi wa Albamu ya Kwaya ya Mt Augustino, Dk Msowoya alisema:

“Ukandamizaji, unyanyasaji wa kimwili, kijinsia, kisaikolojia, au unyanyasaji wa kihisia kwa watoto ni makosa makubwa na yanapaswa kuchukuliwa hatua za kisheria.

Alisema kila mtu ana wajibu wa kutoa usalama na ulinzi kwa watoto na kushirikiana na mamlaka husika kutoa msaada kwa waathirika na kuzuia matukio ya ukatili dhidi ya watoto.

“Watoto wanapaswa kuwa na mazingira salama na yenye upendo ili waweze kukua na kufanikiwa katika maisha yao,” alisema na kuwaomba wananchi pamoja na viongozi wa dini zote kuzungumza na kukemea matukio haya ya ukatili yanayo utia doa mkoa wa Iringa.

“Hii ni hatari, wakati Rais Samia Hassan Suluhu anapambana kuboresha miundo mbinu ya elimu, watoto wanafanyiwa ukatili bila huruma. Sasa tuseme basi,” alisema.

Katika tukio hilo, kwaya ya Mt Augustino wamefanikiwa kuzindua albamu yao ya kwanza yenye nyimbo nane ikibeba jina la Enyi watu wa Mataifa.

Viongozi mbalimbali akiwemo Diwani wa Kata ya Lugalo na Nyalumbu walihudhulia uzinduzi huo ambao ulikusanya zaidi ya kwaya 10 kutoka madhehebu mbalimbali.

3 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *