Mwanajeshi kortini kwa kumkaidi trafiki
Askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ ), MT 89487 CPL Hamis Ramadhan (36) amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam akikabiliwa na mashitaka ya kukataa amri halali ya askari polisi aliyemtaka kusimama katika kivuko cha watembea kwa miguu.
Mshitakiwa huyo amesomewa mashitaka hayo leo na Wakili wa Serikali, Vailet Kyendesa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Rahim Mushi.
Kyendesa alidai mshitakiwa alitenda kosa hilo Februari 7, mwaka huu eneo la Mlimani City barabara ya Survey, Kinondoni, Dar es Salaam.
Alidai mshitakiwa alikuwa akiendesha gari lenye namba za usajili T. 433 ALB aina ya Nissan Patrol, ambapo alisimamishwa eneo la kivuko cha watembea kwa miguu na askari Polisi, lakini alikaidi amri hiyo na kuanza kumsukuma askari kwa gari yake.
Mshitakiwa alikana mashitaka hayo na upande wa mashitaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na kuomba tarehe nyingine kwaajili ya kutajwa.
Hata hivyo, mshitakiwa aliachiwa kwa dhamana. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Machi 6, mwaka huu kwaajili ya kutajwa.