JESHI la Polisi Mkoa wa Iringa linamshikilia Christina Mponzi (34), mkulima mkazi wa Kihesa mjini Iringa baada ya kumkamata akiwa na kete 33 za dawa za kulevya aina ya Heroine.
Mponzi alikutwa na kete hizo katika mkoba wake baada ya wasamalia wema kutoa taarifa hiyo na kufanyiwa upekuzi katika tukio lililotokea hivi karibuni mjini Iringa.
Katika taarifa yake aliyoitoa leo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa ACP Allan Bukumbi alisema; “Tunamshikilia huku tukiendelea na uchunguzi wa tukio hilo.”
Katika tukio lingine, ACP Bukumbi amesema jeshi lake limemkamata Nassoro Mrisho na Consolatha Chonya wakiwa na kilo 73 za dawa za kulevya aina ya bangi.
Alisema dawa hizo zilikamatwa Desemba 18, mwaka huu majira ya saa 5:30 asubuhi zikiwa zimehifadhiwa katika chumba cha Consolatha.
Katika tukio lingine lililotokea Desemba 10, mwaka huu majira ya saa 10:00 jioni katika kijiji cha Kilangali kata ya Image wilayani Kilolo, jeshi la Polisi kwa kushirikiana na askari wa uhifadhi lilimkamata Gwelino Mwanzasi (91) akiwa na silaha nne aina ya Gobole na Shortgun moja.
Aidha mtuhumiwa huyo alikutwa na gololi 30 za gobole, risini nne za shortgun, baruti ujazo wa nusu lita, jino la kiboko, kipande cha ngozi ya nyati, gamba la kakakuona na risasi za silaha mbalimbali.
“Pia katika oparesheni tunazoendelea kufanya ndani ya manispaa ya Iringa ambayo imelenga kuwakamata watu wanaojihusisha na vitendo vya uporaji, tumafanikiwa kuwakamata watuhumiwa nane wakiwa na mali mbalimbali za wizi, mapanga matano, vifaa vya kuvunjia pamoja na vipande vya nondo,” alisema.