MWANDISHI mkongwe mstaafu wa Magazeti ya Serikali ya Daily News na Sunday News, Charles Kizigha (72) anatarajiwa kuzikwa Ijumaa wiki hii, Dar es Salaam.
Kizigha aliaga dunia Agosti 27 mwaka huu baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Akizungumza na HabariLEO, Jumapili, kuhusu taratibu za mazishi, Mwenyekiti wa Kamati ya mazishi , Isaac Mruma alisema Kizigha atazikwa Ijumaa Septemba 2, mwaka huu jijini Dar es Salaam.
“Taratibu za msiba wa Kizigha zinaendelea nyumbani kwake Mbezi Beach -Africana na hadi sasa kikao cha familia kimekubali marehemu atazikwa hapa Dar es Salaam Ijumaa wiki hii. Maziko yatafanywa katika makaburi ya Kondo, kama kutakuwa na mabadiliko ya makaburi kuwa ya Kinondoni tutatoa taarifa,”alisema Mruma.
Mruma alisema Kizigha alikuwa akitibiwa muda mrefu katika Hospitali ya Mzena, Dar es Salaam na Agosti 19 mwaka huu alilazwa hospitalini hapo akiendelea na matibabu na Agosti 27 jioni alifariki.
Alisema mwili wa marehemu utalala nyumbani Alhamisi na Ijumaa asubuhi kutakuwa na ibada fupi nyumbani hapo na mwili huo utapelekwa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT)-Usharika wa Mbezi Beach kwa ajili ya ibada ya mazishi.
Mruma alisema baada ya ibada mwili utapelekwa makaburini kwa ajili ya maziko.
Kizigha ameacha mke, watoto watatu na wajukuu. Alizaliwa Oktoba 11 mwaka 1950.
Kizigha alikuwa gwiji wa habari za uchunguzi na pia amekuwa mtumishi wa muda mrefu katika magazeti hayo ya Daily News na Sunday News hadi anastaafu.
Mhariri Mtendaji wa zamami wa TSN, Charles Rajabu alisema alianza kufahamiana na Kizigha mwaka 1972.
“Nilihamishwa kutoka gazeti la The Nationalist na Standard kwenda kuunda gazeti la Daily News mwaka 1972 ndipo nikakutana na Kizigha wakati huo tukiwa vijana wadogo,”alisema Rajabu.
Alisema wakati huo ndio alikuwa ametoka kusoma Nairobi na yeye na Kizigha walikuwa waandishi wa habari vijana.
“Nilifanya nae kazi wakati huo nikaanza kupanda hadi nikateuliwa na Rais Ali Hassan Mwinyi kuwa Mhariri Mtendaji wa TSN mwaka 1990, ndipo nilipomjua zaidi Kizigha, akawa tunampa kazi za uchunguzi zaidi kwa kuwa alizipenda,”alisema Rajabu.
Alisema Kizigha alikuwa mchapakazi na mwandishi nguli aliyejituma na kuwa aliishi nae kwenye jengo moja la makazi eneo la Sea View Dar es Salaam hadi yeye Rajabu alipohamishiwa kituo cha kazi kwenda Idara ya Habari, Maelezo na baadaye Wizara ya Habari hadi alipostaafu mwaka 2009.
“Alitumia muda mwingi ofisini, alifanya habari za uchunguzi, alizipenda, asubuhi ukifika, unamkuta ameshafika anapiga simu zake kutafuta habari, kwa kweli tumepoteza mwanahabari nguli,”alisema Rajabu.