Mwangaza sheria ya mtoto kudhibiti ukatili

UELEWA duni pamoja na kupuuzwa kwa sheria ya mtoto ya mwaka 2009 miongoni mwa wazazi, walezi na taasisi imetajwa kuwa kiini kikubwa cha ongezeko la matukio ya ukatili dhidi ya watoto mkoani Geita.

Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Mkoa wa Geita, Paulina Majogoro amesema hayo katika mahafari ya 11 ya kidato cha nne ya shule ya sekondari ya Geita Adventist iliyopo mjini Geita.

Amesema changamoto hiyo inaashiria kuna uhitaji mkubwa wa elimu na msisitizo wa sheria ya mtoto kwenye familia na jamii ili kuimarisha usalama na usimamizi wa ulinzi wa kisheria wa haki ya mtoto.

Ameeleza, wapo wazazi wanaamini mtoto anapohitimu elimu ya msingi ama sekondari yupo tayari kujitegemea ingali ana umri chini ya miaka 18 na kupelekea watoto wengi wa kike kuwa hatarini zaidi.

“Jukumu la kwanza la wahitimu ni kwenda kuyaishi yale waliyolelewa na yale waliyofundishwa, jukumu la pili ni wazazi bado wanayo nafasi ya kutoa elimu ya kuendeleza maadili kwa watoto wao.

“Wasiwaache watoto holela eti kwa sababu wamemaliza kidato cha nne, lakini jukumu la tatu bado ni la jamii nzima kuhakikisha watoto wetu hawa wanaokuja basi wanakuwa kwenye mazingira salama.

“Kwa hiyo tujitahidi kama jamii tunashirikiana pamoja tunapambana hii vita ya kuwalinda watoto wetu ya kuhakikisha wako salama na hili jukumu siyo la mtu mmoja ni la wazazi, walimu, serikali na kila mtu.

Mkurugenzi wa Shule za Geita Adventist, George Hezrone amesema jumla ya wanafunzi 234 wamefanya mahafari ya kuhitimu kidato cha nne ambapo wamejengwa zaidi katika elimu ya kidini na kitaaluma.

Amesema pia shule za Geita Adventist zimewekeza kuwafundisha watoto haki zao ili wapate ufahamu na ujasiri wa kujilinda dhidi ya viashiria na vitendo vya ukatili wawapo shuleni, nyumbani na mtaani.

“Sheria ya watoto ya nchi yetu na ile ya kimataifa tunajitahidi sana kuwafanya walimu wetu wawafundishe watoto wajue haki zao ambazo zipo kwenye sheria na katiba ya nchi yetu.

“Tumejikita sana kuwalea kiroho na kuwafanya sana waijue imani ya dini, kila mmoja kwa imani yake, kwa mantiki hiyo inawasaidia kufahamu kwamba dhambi ya aina yeyote matokeo yake ni kifo.

Mmoja ya wazazi wa wahitimu wa shule hiyo, Juma Jumanne ameeleza kiini cha tatizo ni ulegevu wa malezi ya wazazi huku kutozingatiwa sheria ya mtoto chanzo ni uelewa duni wa jamii juu ya sheria hiyo.

Habari Zifananazo

Back to top button