Mwanza yazidi kuunganishwa miundombinu bora ya usafiri

MWANZA imeendelea kuunganishwa kwa miundombinu ya usafiri wa uhakika kwa uwepo wa barabara na vivuko kama ilivyo mishipa ya damu iliyozunguka mwili wa binadamu ikisukuma damu na kuwezesha uhai wa mtu.

Hivi karibuni serikali imesaini mikataba ya ujenzi wa miundombinu ya usafiri kwa zaidi ya Sh bilioni 77 mkoani humo kujenga barabara ya lami ya urefu wa kilometa 54.4 kutoka Sengerema kwenda Nyehunge na kivuko cha Buyagu (Sengerema) kwenda Mbalika (Misungwi) kwa ajili ya kuvusha watu na bidhaa.

Katika utiaji saini huo uliohudhuriwa na wananchi wengi katika viwanja vya Sabasaba wilayani Sengerema, Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Godfrey Kasekenya, alisema dhamira ya serikali ni kutaka nchi kufunguliwa kwa kuwa na miundombinu bora.

Kasekenya alisema ujenzi wa barabara kutoka Sengerema kwenda Nyehunge utagharimu Sh bilioni 73.4 na kivuko kitagharimu Sh bilioni 3.8 na zinatoka serikalini kwa asilimia 100.

“Haya ni mageuzi makubwa kwani maendeleo yanapatikana pale panapokuwa na uhakika wa usafiri ndio maana unaona juhudi kubwa hizi za kuwekeza zilizofanywa hapa,” alisema Kasekenya.

Alisema lengo la Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha kuwa maeneo yote yanaunganishwa kwa kujengwa kwa barabara za lami mkoa hadi mkoa na katika maeneo ya Ziwa Victoria kunakuwepo kwa uhakika wa vivuko na usafiri wa meli.

Kasekenya alisema kwa vile Ziwa Victoria linaunganisha mikoa mingi ya Kanda ya Ziwa serikali inaendelea na jitihada za kuhakikisha inaweka vivuko sehemu isiyo navyo vibovu vinakarabatiwa ili kuwezesha usalama wa watu na bidhaa.

“Tumefufua Mv Clarius ili itoe huduma ya kuunganisha maeneo mengi ya visiwa vilivyopo ndani ya Ziwa Victoria ili wananchi wamudu kuvuka kupata mahitaji yao kwa usalama,” alisema Kasekenya.

Alisema nchi ina barabara za urefu wa kilometa zaidi ya 36,000 huku mpaka sasa kilometa zaidi ya 12,000 zikiwa zimeunganishwa kwa lami.

Alisema katika kuhakikisha kuwa mafanikio makubwa yanafikiwa katika sekta ya usafiri daraja la urefu wa kilometa 3.2 la Kigongo Busisi maarufu Daraja la JP Magufuli limefikia asilimia 72 huku fedha zote za ujenzi zaidi ya Sh bilioni 716 zikiwa tayari zimelipwa kwa mkandarasi.

Naibu Waziri huyo alisema jitihada hizo za kuunganisha sehemu zote kwa kuwa na mtandao wa usafiri wa uhakika vilevile imeelekezwa katika ujenzi wa meli za kisasa zenye uwezo wa kubeba abiria wengi.

Hivi karibuni meli ya Mv Mwanza Hapa Kazi Tu itakayokuwa na uwezo wa kubeba abiria 1,200, tani 400 za mizigo, magari 20 ambayo vilevile itakuwa na ukumbi wa mikutano itaanza kutoa huduma za usafiri wa watu na bidhaa ndani ya Ziwa Victoria.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima aliishukuru serikali kwa kuwezesha miradi hiyo na kusema hakika itasaidia kuondoa changamoto zilizokuwepo katika maeneo hayo.

Alisema miradi hiyo iliyoanzishwa ni ya kimkakati kwani wananchi watanufaika kwa kusafirisha mizigo yao kwa wepesi na abiria wakiwa na uhakika wa usalama wao wawapo majini.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi wa Umeme (TEMESA), Lazaro Kilahala anasema ujenzi wa kivuko hicho cha Buyagu kwenda Mbalika itafanywa na Kampuni ya Songoro Marine ya jijini Mwanza na kazi hiyo inatarajiwa kukamilika baada ya miezi 10.

Alisema vilevile Temesa inaendelea na ukarabati wa vivuko vingine vitano kwa bilioni 33.2.

Kilahala alisema Temesa itasimamia kuhakikisha ujenzi wa vivuko hivyo inafanywa kwa mafanikio na ubora mkubwa wa kuhudumia watu.

Naye Mkurugenzi wa Songoro Marine, Meja Songoro, aliipongeza serikali kwa kuwaamini kuwatumia wakandarasi wazalendo katika ujenzi wa miradi ya vivuko inayoendelea nchini.

Songoro aliahidi kufanya kazi aliyopewa kwa uadilifu kuendana na muda wa mkataba ulivyo ili kuwezesha Watanzania kufaidi jitihada wanazofanyiwa na serikali yao.

Naye Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Rogatus Mativila anasema kusainiwa kwa mkataba wa ujenzi wa barabara hiyo itawezesha kuunganisha maeneo hayo na mikoa jirani ya Kagera, Kigoma na Geita.

Anasema ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami kwa urefu wa kilometa 54.4 unafanywa na AVM Dillingham Construction International ya Uturuki ambapo kazi itakamilika miezi 28 na itachochea ukuaji wa uchumi katika maeneo hayo.

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jamal Abdulbabu, alipongeza jitihada hizo akisema ujenzi huo ni utekelezaji wa Ilani ya chama hicho ya mwaka 2020-2025.

Abdulbabu alisema kuendelea kutatuliwa kwa kero za wananchi ni hatua nzuri kwa jamii kufikia kwenye hatua nzuri ya kimaendeleo nchini.

Alisema suala la kutengeneza vivuko ni moja ya kipaumbele kilichoainishwa ili maeneo yote yaunganishwe na kupitika kwa uhakika.

Alimshukuru Rais Samia kuguswa na hitaji la barabara katika eneo hilo na kuamua kutekeleza ahadi ya mtangulizi wake, Dk John Magufuli na serikali yake kusaini kuanza ujenzi wa barabara hiyo kwa lami.

Abdulbabu alisema kuwa Rais Dk Samia ameonesha kwa vitendo mgawanyo wa huduma za kijamii katika maeneo yote nchini kwani kila sehemu pamefikiwa na huduma za kijamii.

“Bila kuwepo kwa uwekezaji wa vivuko ingekuwa ni shida katika maeneo ya visiwa angalia Ukerewe ina visiwa 38 hivyo bila vivuko ingekuwa shida kwa wananchi hao,” alisema Abdulbabu.

Baadhi ya vivuko ambavyo viko karibu kukamilika ni ya Bwiro-Bukondo, Nyakalilo-Kome na Ijinga-Kahangala kuwezesha kupatikana kwa upitaji rahisi wa kwenda na kurudi Sengerema, Magu na Ukerewe.

Mbunge wa Sengerema, Hamis Tabasamu alipongeza hatua hiyo akisema kuwa ilikuwa inamnyima usingizi kwa muda mrefu kwani wananchi walikuwa wanapata changamoto ya usafiri hivyo ujenzi huo ukikamilika watatumia muda mfupi kusafiri kupitia eneo hilo.

Aliwataka wananchi katika maeneo ambayo mradi huo utapita kuwa walinzi wa vifaa vya ujenzi kwa kuwa ni sehemu ya kodi zao zinatumika.

Habari Zifananazo

Back to top button