Mwarobaini tatizo la umeme watajwa

Mchezo wa manati wachangia adha ya umeme Mtwara

SERIKALI imetenga jumla ya Shilingi bilioni 250 kujenga Gridi ya Taifa kutoka Songea –Tunduru – hadi Masasi katika kipindi cha mwaka wa fedha 2022/2023, kwa lengo la kukabiliana na adha ya kukatika kwa umeme.

Aidha, kiasi cha Shilingi Bilioni 66.7 zimetengwa kwa lengo la kuanza ujenzi wa njia hiyo.

Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato ameweka bayana mipango hiyo ya serikali bungeni, Dodoma leo asubuhi wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Ndanda, Cecil Mwambe aliyetaka kujua  mkakati wa serikali ya kumaliza kero ya kukatika kwa umeme mara kwa mara kwa mikoa ya Kusini hasa wilayani Masasi.

Advertisement

Mbali na mpango huo wa kudumu wa taifa zima, Wakili Byabato amelieleza Bunge katika kutekeleza mpango mahususi kwa ajili ya mikoa ya Kusini, serikali imetenga kiasi cha Shilingi milioni 600 kwa ajili ya kurekebisha miundombinu katika njia za umeme Newala, Nyangao,Masasi na Mahuta.

“Aidha, jumla ya Shilingi bilioni 2.2 zimetengwa kwa ajili ya kujenga njia ya umeme ya msongo wa kilovoti 33 kutoka Nanganga hadi Masasi,” Naibu Waziri ameeleza.

Kwa mujibu wa Byabato, kiasi cha Shilingi bilioni  mbili kimetengwa kuweka transfoma kubwa kati ya Tunduru na  Namtumbo ili kupata umeme mkubwa kutoka Ruvuma bila kuathiri watumiaji wengine.