Mwekezaji Singida alia na mgogoro uliodumu miaka 28

MWEKEZAJI mzawa Leonard Suih, aliyejenga majengo ya biashara ya kitega uchumi yenye thamani ya Shilingi milioni 700 mkoani Singida, amemuomba Rais Samia Suluhu Hassan, kuingilia kati mgogoro baina yake na Manispaa ya Singida uliodumu kwa zaidi ya miaka 28.

Suih alisema hayo wakati alipozungumza na waandishi wa habari jijini hapa kwa lengo la kufikisha kilio chake kwa Rais Samia kuomba asibomolewe majengo yake baada ya uongozi wa mkoa huo kutaka kubomoa majengo manne na hivyo kupoteza haki yake.

Alisema mgogoro huo umedumu kwa miaka zaidi ya 28, na umekuwa ukiibuka na kupoa mara kwa mara hali ambayo inasababisha ashindwe kutekeleza majukumu yake kwa amani na kumuathiri kisaikolojia.

Akizungumzia mgogoro huo alisema miaka 28 iliyopita alipatiwa eneo na Manispaa ya Singida, ambalo lilikuwa dampo katika stendi ya mabasi ya zamani na kulazimika kulisafisha ili kufanya uwekezaji huo.

“Miaka ya nyuma mkoa wa Singida ulikuwa na tatizo la kuibuka kipindupindu kila mara na sababu kubwa ilikuwa ni lile dampo mimi nikaliomba eneo lile ambalo lilikuwa dampo tukakubaliana tukafikia makubaliano, lakini kuondolewa taka zilizokuwepo ilikuwa inahitajika milioni sita kwa wakati huo sio fedha ndogo.

“Milioni hizo sita Manispaa wao walidai kuwa hawana bajeti ikabidi mimi ndiye nigharamie ikabidi nifanyie hivyo kwa makubalino kuwa watanirejeshea nikatoa uchafu ule kama tani 1,500 na kuanza maandalizi ya ujenzi na toka wakati huo kipindupindu kikaisha Singida,”alisema.

Alisema baada ya kumaliza kuondoa uchafu katika dampo hilo manispaa walishindwa kumlipa fedha alizotumia, hivyo wakalazimika kummilikisha sehemu ya eneo hilo ambalo alijenga majengo ya biashara ikiwemo choo na bafu ya kulipia.

Alisema eneo hilo pamoja na kujenga choo na bafu cha kulipia aliwekeza pia majengo ya biashara manne ambayo yaligharimu takribani Sh milioni 700, na kuanza kufanya biashara zake.

“Hivi juzi nilikuwa nafanya ukarabati kidogo wa kubadili paa lilikuwa limechoka akaja mhandisi wa Manispaa na akasema nisifanye lolote nisimamishe ujenzi nikaomba basi nirudishie hata mabati, ili bidhaa zisinyeshewe akasema hakuna kufanya lolote, matokeo yake mvua ikaharibu bidhaa zilizikuwepo na picha ninazo hapa,”alisema.

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba alipoulizwa kuhusu malalamiko hayo kwa njia ya simu alisema, mkataba baina ya Manispaa ya Singida na mwekezaji huyo unamtaka kutofanya jambo lolote hadi apatiwe kibali.

“Lile ni eneo la ubia baina ya manispaa na mwekezaji sasa hawezi kufanya kitu bila sisi kujua ili kama kuna gharama ametumia tujue na mkataba wake upo mwisho unakwisha 2025 tumemwambia aandike barua lakini hataki kwa nini?” Alihoji Serukamba.

Hata hivyo, alisema kinachofanywa na mkoa ni kwa mujibu wa mkataba ambao walikubaliana pande zote mbili lakini mwekezaji anaonekana hataki kuufuata na kufanya kinyume na makubaliano yao.

“Tulishaongea naye mbele ya mke wake akasema anakwenda kuandika barua lakini hadi leo hajaleta barua kwanini, yeye alete barua ya kuomba kibali na sisi tutampatia ruhusa ya kufanya kile anachotaka” alisema Serukamba.

Habari Zifananazo

Back to top button