Mwendokasi Mbagala, G/Mboto kuanza Februari-Machi 2025
DAR ES SALAAM: NAIBU Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Zainabu Katimba amewataka Wakandarasi wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) kuhakikisha huduma ya mabasi yanaanza kama ilivyokubaliwa ili wananchi wapate huduma.
Akiwa katika ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kukagua ujenzi wa mradi wa mabasi yaendayo haraka jijini Dar es Salaam, Katimba amesema miradi ya awamu ya pili na ya tatu kwa safari za Gerezani-Mbagala imefikia asilimia 98.9 na ile ya Barabara ya Nyerere kuelekea Gongolamboto imefikia asilimia 50.
“Tunajua kuna changamoto ya mvua. Serikali ni sikivu imewaongezea muda wakandarasi wa Barabara ya Nyerere, hivyo mnapaswa kukamilisha ndani ya muda tuliyokubaliana,” amesema kiongozi huyo.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Ofisi ya Rais (TAMISEMI), Justin Nyamoga amesema ameridhishwa na mwenendo wa ujenzi katika maeneo waliyotembelea ingawa amewaasa viongozi DART kuharakisha huduma ya usafiri wa mwendokasi unakamilika haraka kuwahudumia wananchi wa maeneo hayo.
Naye, Mtendaji Mkuu wa DART, Dk Athumani Kihamia amesema amepokea mapendekezo na ushauri kutoka kamati hiyo ya bunge pia kufikia mwezi Februari mwakani huduma ya usafiri wa mwendokasi utaanza kwa safari ya Gerezani-Mbagala.
Pia, kufikia mwezi Machi 2025 huduma ya safari za mabasi ya mwendokasi yataanza katika Barabara ya Nyerere hadi kuwafutia wananchi wa maeneo ya Gongolamboto.
Aidha, amesema kinachopelekea kuchelewa kwa huduma hiyo ni hatua za upatikanaji wa mabasi hayo ambayo hutengenezwa kwa oda maalumu nje ya nchi.