Mwenge kupitia miradi ya Sh bilioni 30 Mtwara

MTWARA: MIRADI 62 ya maendeleo itapitiwa na Mwenge wa Uhuru mkoani Mtwara yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 30 mwaka 2024.

Akizungumza leo mkoani Mtwara baada ya kuwasili kwa Mwenge huo wa Uhuru ukitokea mkoani Lindi, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala amesema Mwenge utakimbizwa katika njia zenye urefu wa kilometa 906.6.

Hata hivyo unakimbizwa katika halmashauri 9 ambapo pamoja na kazi nyingine unatarajia kuweka mawe ya msingi katika miradi 22, kufungua miradi 2 na kuzindua miradi 11.

Pia kuona na kukagua miradi 27 ambapo hiyo yote inatekelezwa na wananchi kwa kushirikiana na serikali kuu, wahisani pamoja na halmshauri kwa ujumla.

SOMA: Mwenge kukagua miradi 87 Tanga

“Mbio hizi za Mwenge wa Uhuru mwaka huu zitawakumbusha wananchi kuhusu haki yao ya kikatiba ya kushiriki kuchagua, kuchaguliwa kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajia kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu,” amesema Sawala

Amesema kupitia mbio hizo wananchi watapata fursa ya kujengewa uwelewa zaidi kuhusu masuala mbalimbali ikiwemo uhifadhi wa mazingira hivyo kukabiliana vema na athari za mabadiliko ya tabia ya nchi yanayokabili dunia, taifa na mkoa kwa ujumla.

Aidha Mwenge huo wa Uhuru umeanza kukimbizwa leo Mei 30, 2024 katika manispaa ya mtwara mikindani mkoani humo ambapo jumla ya miradi mbalimbali 6 ya maendeleo itapitiwa yenye thamani ya Sh bilioni 1.3.

Akitoa taarifa ya mbio za Mwenge huo wa Uhuru katika manispaa hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mwanahamisi Munkunda amesema mwenge utakimbizwa kwenye umbali wa kilometa 70 na utaweka mawe ya msingi miradi 3 ya maendeleo, kuzindua miradi 2 pamoja na kutembelea na kukagua mradi 1.

Mwenge wa Uhuru mkoani humo umepokelewa katika kijiji cha mpapura halmashauri ya wilaya ya mtwara.

Kauli mbiu ya mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu inasema ‘Tunza Mazingira na Shiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa Ujenzi wa Taifa endelevu’.

 

Habari Zifananazo

Back to top button