Mwenge kuweka jiwe la msingi miradi Sh bilioni 1 Newala

MWENGE wa Uhuru umekabidhiwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Newala mkoani Mtwara baada ya kumaliza mbio zake katika Halmashauri ya Mji wa Newala ambapo itatembelea na kuweka Jiwe la Msingi miradi mbalimbali ya maendeleo huko yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 1.
Akikabidhi mwenge huo leo Aprili 7, 2023 kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Newala, Shamimu Daudi amesema katika halmashauri yake Mwenge uliona, kukagua, kuweka jiwe la msingi na kuzindua jumla ya miradi sita ya maendeleo yenye thamani ya Sh Bilioni 4.
Miradi iliyotembelewa na kuwekewa jiwe la msingi ikiwemo sekta ya afya, maji, barabara, elimu, kikundi cha wajasiliamali na mingine.
Amesema Mwenge wa Uhuru katika halmashauri hiyo umeridhia miradi yote iliyotembelewa na kuwekewa jiwe la msingi kwenye halmashauri hiyo miradi ambayo Mwenge wa Uhuru imetoa maelekezo ikiwa ni pamoja na kuwasimamia wakandarasi wanaojenga miradi ya barabara ambapo watatekeleza maagizo hayo.
Akipokea mwenge huo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala, Duncan Tebas amesema katika halmshauri yake Mwenge wa Uhuru utatembelea, kuweka jiwe la msingi jumla ya miradi 7 ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya Sh Bilioni 1.
Aidha Mwenge wa Uhuru umeweka jiwe la msingi katika mradi wa wa barabara ya Kitangari-Mtongwele yenye urefu wa kilomita 1.2 kiwango cha lami unaogharimu Sh milioni 600 chini ya Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) wilayani humo.
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Abdalla Shaib Kaim ameridhia kuweka Jiwe la Msingi katika mradi huo wa barabara wa Kitangari-Mtongwele kwani umekidhi vigezo na ubora na kuwataka wasimamizi wa miradi kwamba wanapopewa fedha kwa ajili ya kukekeza miradi hiyo ya maendeleo wasifanye kwasababu Mwenge wa Uhuru unakuja wafanye kwa ajili ya Watanzania wote .
Baadhi ya wananchi wa kijiji hicho cha Kitangari wilayani humo “Tunaishukuru Serikali yetu kwa kutuletea mradi huu wa barabara kwa kiwango cha lami kwani sasa hivi tumeondokana na kero ya barabara iliyokuwa inatukabili kwa miaka mingi hapa Kijijini kwetu tulikuwa tabu sana hasa kipindi cha mvua ikuwa hapitiki kabisa”, Amesema Zaibu Issa.