Mwenge wa Uhuru waingia Lindi

MWENGE wa Uhuru umemaliza mbio zake mkoani Mtwara na kukabidhiwa Kijiji cha Nyangao kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Mtama mkoani Lindi, baada ya kukagua miradi 54 yenye thamani zaidi ya Sh bilioni 31 Mtwara.

Akizungumza leo wakati akikabidhi mwenge huo kwa Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telack, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Ahmed Abbas amesema mbio za Mwenge wa Uhuru ukiwa mkoani Mtwara umekimbizwa katika halmashauri tisa na urefu wa kilometa 948.6.

Amesema pamoja na kazi nyingine Mwenge wa Uhuru umeweka Jiwe la Msingi miradi 20, kufungua miradi sita, kuzindua miradi 10, kuona na kukagua miradi 18 inayotekelezwa na wananchi kwa kushirikiana na Serikali, wahisani pamoja na halmashauri.

Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Abdalla Shaib Kaim wakati akiondoka mkoani humo ameupongeza uongozi wa Mkoa wa Mtwara kwa kazi kubwa na mzuri waliyoifanya katika usimamiza wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

“Mwenge wa Uhuru umekagua miradi na kujiridhisha kazi mumesisamia vizuri miwapongeze usimamizi wa Mkoa nasema hongereni sana,” amesema Kaim.

Ameutaka uongozi wa Mkoa huo kuendelea kufanya kazi kwa uzalendo, kwani kinachohitajika ni jitihada kubwa za kuisaidia Serikali katika kutimiza azima ya wananchi hasa masuala mbalimbali ya maendeleo.

Ameupongeza uongozi huo katika suala zima la utunzaji wa mazingira, kwani wameunga mkono kauli mbiu ya Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2023, hivyo kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini waendelee kupanda miti kwa ajili ya kuhifadhi mazingira

Kauli mbiu ya Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2023 inasema: Tunza Mazingira, Okoa Vyanzo vya Maji kwa Ustawi wa Viumbe Hai na Uchumi wa Taifa

Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2023 zilizinduliwa Kitaifa Aprili 1, mwaka huu mkoani Mtwara na Waziri Mkuu , Kassim Majaliwa.

Habari Zifananazo

Back to top button