DSM; KIJANA Malick Hamis (24) mwenye ulemavu wa macho amebuni mfumo wa kupakua sauti kwa kutumia kompyuta na kuziunganisha, jambo linaloonesha kukua kwa teknolojia kwa makundi mbalimbali katika jamii.
Akizungumza leo Dar es Salaam katika kongamano la saba la TEHAMA (TAIC), lilioandaliwa na Tume ya Tehama nchini (ICTC), Malick alisema lengo lake ni kubobea katika suala zima la ubunifu kwenye Tehama.
Amesema alianza matatizo ya macho akiwa darasa la tatu na katika harakati za kufuatilia matibabu alishindwa kumaliza darasa la saba na kuishia la sita.
” Licha ya kutomaliza shule lakini nilisikia taarifa kuwa mtu asiyeona anaweza kupata elimu ,” amesema na kuongeza kuwa ndipo alipojiunga na elimu saidizi inayotolewa na Chuo Kikuu Huria (OUT) na kuanza masomo mwaka 2019.
Amesema aliendelea kusoma masuala ya kompyuta na mwaka huu 2023 alihitimu na kupewa vyeti.
Amesema pamoja na kuwa na ubunifu wa kuunganisha sauti, lakini pia anajifunza kutumia kompyuta kuhariri (editing)katika nyanja balimbali na katika kupakua mfumo wa sauti amepakua sauti za baadhi ya viongozi wakuu wa serikali.
Kwa upande wake Faraja Mwansasu ambaye naye ni mlemavu wa macho ameisihi serikali kuhakikisha kuwa na vifaa jumuishi kwa kundi hilo.