Mwenyekiti CCM Iringa atoa maelekezo mapato ya vijiji

MWENYEKITI wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa, Daudi Yassin ameelekeza viongozi wa chama hicho wa Kata na vijiji vyote mkoani mwake kuhakikisha serikali za vijiji zinatoa kwa wakati taarifa za mapato na matumizi kwa wananchi.

Pamoja na taarifa hiyo amewataka viongozi hao na ngazi nyingine zote mkoani humo kutoa taarifa za utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika maeneo yao.

“Nawaagiza viongozi wote wa chama katika mikutano yoyote watakayofanya mijini na vijijini swali lao la kwanza kwa wananchi lihusu kama wanapata taarifa mapato na matumizi kwa maana ya nini wanapokea au wamekusanya katika maeneo yao na yametumikaje,” alisema mapema leo wakati akifungua kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Iringa.

Alisema iwe mwiko kwa wana CCM kutetea viongozi wabadhirifu katika maeneo yao na kwa kufanya hivyo watakiweka chama katika mazingira mazuri ya kuendelea kujipatia ushindi wa kishindo katika chaguzi mbalimbali za serikali.

Katika kikao hicho kilichohudhuriwa na wajumbe 126, Yassin alisema viongozi wa chama hicho na wanachama wake wanapaswa kuwa vinara wa kuimba kazi zinazofanywa na serikali yao.

“Changamoto zetu kama chama hizo tutazimaliza kwenye vikao vyetu vya ndani. Huko nje twende na taarifa za utekelezaji wa Ilani yetu, kazi zinazofanywa na serikali ni nyingi lakini hazitangazwi inavyotakiwa,” alisema na kuwatahadharisha viongozi wa chama hicho wanaokwenda kwenye vyombo vya habari na kukikosoa chama chao.

Aliipongeza serikali ya Dk Samia Suluhu Hassan akisema kwa miaka miwili madarakani imefanya kazi kubwa za maendeleo katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, barabara, maji, kilimo, uwekezaji na elimu.

“Kila mahali kuna mradi umejengwa ndani ya miaka hii miwili ya Mama Samia. Rudini mkawaoneshe wasioona ili waone,” alisema.

Aidha alizungumzia maridhiano ya kisiasa yanayoendelea baina ya serikali ya CCM na vyama vya upinzani akisema: “Yanatufanya tuwe wamoja katika kuiletea nchi maendeleo na yanaongeza mshikamano na amani katika Taifa hili.”

Habari Zifananazo

Back to top button