Mwenyekiti CCM Katavi hataki viongozi legelege

MWENYEKITI Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Katavi, Idd Kimanta, amewataka viongozi wa chama hicho wilayani Mpanda kufanya kazi kwa weledi  na kuimarisha chama.

Kimanta ametoa kauli hiyo katika kikao kazi kilichofanyika kwa wanachama wa CCM Wilaya ya Mpanda katika ziara yake ya kutembelea wilaya zote za Mkoa wa Katavi.

Kimanta ameahidi uongozi shirikishi kwa viongozi wenzake na kutaka kila mtu kuheshimu uongozi wa mwenzake na kutekeleza majukumu yake kwa kujiamini na kukataa viongozi legelege, wasioweza kutoa uamuzi katika ngazi zao za matawi na kata.

“CCM ndio kimbilio la wanyonge na nitashughulika na viongozi legelege kupitia vikao kazi na tutamjadili mtu kwa utendaji kazi wake na sio kwa chuki na nimenyooka kama rula kwenye mambo ya msingi ya kukijenga chama,”amesisitiza Kimanta.

Amewataka viongozi kutatua kero za wananchi, badala ya kuwa viongozi wa kushabikia kero, kwani kuwa kiongozi ni mfano wa kuigwa na kuitetea serikali pale inaposhambuliwa.

Awali katika kikao kazi hicho kilichohudhuriwa na wanachama wa CCM kutoka Kata 27 za Wilaya ya Mpanda, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mpanda Method Mtepa, aliwataka wanachama kupendana na kuacha tabia ya chuki.

Akitoa salamu kwa niaba ya wabunge wa Wilaya ya Mpand,a Mbunge Sebastian Kapufi aliwaahidi wanachama wa CCM kuendelea kutekeleza Ilani ya CCM na kupigania maendeleo ya miradi inayotekelezwa katika wilaya hiyo.

Habari Zifananazo

Back to top button