Mwenyekiti Moita atuhumiwa matumizi ya ardhi bila ridhaa

BAADHI ya wananchi wa kijiji cha Kilimatinde Wilaya ya Arumeru Mkoa wa Arusha na wa kijiji cha Moita Bwawani Wilaya ya Monduli wanamtuhumiwa mwenyekiti wa kijiji cha Moita, Bruno Mollel kwa kumega ardhi ya malisho ekari 3,000 kuwa eneo la makazi bila ridhaa ya wananchi.

Wakizungumza katika mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na watu zaidi ya 150 uliofanyika katika kijiji cha Moita Bwawani walisema na kuiomba serikali kusitisha zoezi hilo kwa kuwa mwenyekiti huyo hajali wananchi wenye mifugo kwani eneo hilo lilitengwa kwa ajili ya malisho ya mifugo.

Mmoja wa wananchi hao aliyejitambuylisha kwa jina la Ndoipo Mollel maarufu kwa jina la ‘’Ndoipo Maskini Mollel’’ alisema kitendo kilichofanywa na mwenyekiti kinapaswa kulaaniwa kwa kuwa alijali maslahi yake na sio ya wafugaji.

Advertisement

Mollel alisema ardhi ni ya watanzania wote na sio ya baadhi ya vijiji hivyo wao wanaungana na wananchi wa vijiji vingine kupinga kumegwa kwa ardhi hiyo ili eneo hilo liendelee kuwa eneo la malisho na sio vinginevyo.

Mwanakijiji mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Ndekui Laizer alisema kuwa utaratibu uliotumia mwenyekiti Mollel wa kumega ardhi kwa ajili ya makazi sio sahihi kwani hakujali na kuzingatia maslahi ya wafugaji juu ya kutengwa eneo hilo kwa ajili ya malisho.

Alisema mwenyekiti huyo ameweka mbele tamaa zake na maslahi yake binafsi bila kuzingatia jamii anayoiongoza inayojali eneo la malisho kuliko makazi hivyo maazimio yote yaliyopitishwa yanapaswa kusitishwa na kubadilishwa kwa maslahi ya wananchi wa vijiji vyote vya Arumeru na Monduli.

Akijibu tuhuma hizo, Mwenyekiti Mollel alisema chokochoko zote za wananchi wa Kilimatinde na Moita zinachochewa na mwanasiasa na mfanyabiashara wa madini, Sanare Mollel na kudai kuwa maamuzi ya wengi yamezingatia na ndio maana serikali ilitoa hati ya ardhi kwa ajili ya kumega eneo la malisho kwa ajili ya makazi.

Mollel alisema kuwa vikao vya kijiji na halmashauri ya kijiji vilikaa na kupata baraka ngazi ya wilaya hivyo wale baadhi ya wote  wanaopinga utoaji wa ardhi kwa ajili ya makazi hawana hoja za msingi kwa kuwa serikali ilishabariki na hatimaye kuridhia utoaji wa ardhi hiyo.

Akijibu tuhuma za mwenyekiti kuwa yeye anachochoe vurugu za kupinga utoaji ardhi ya malisho kwa ajili ya makazi mfanyabiashara Sanare Mollel alisema ni hoja dhaifu zisizo na mashiko na kusema kuwa wananchi wenye wameamua kutetea eneo hilo kwa ajili ya malisho.

Mollel alisema watanzania wa sasa hususani wafugaji wa jamii ya kimasai wamekuwa welevu na wenye kujua thamani ya eneo la malisho hivyo kumega kwa ajili ya makazi sio hoja yenye mashiko kwani taratibu zote hazikufuatwa hivyo aliiomba serikali kuhakikisha hilo linasitishwa kw amaslahi ya wananchi wa Moita na vijiji vya jirani.

Mfanyabiashara huyo aliwataka viongozi wa Moita kujibu hoja za wananchi na sio kumsingizia yeye eti naleta chokochoko na vurugu kwani wananchi wa jamii ya kifugaji wanajali eneo la malisho kuliko makazi.

Naye Katibu Tawala wa Wilaya ya Monduli aliyetambuliwa kwa jina la Mbise aliwaeleza wananchi hao kuwa suala lao liko mikononi mwa Mkuu wa Wilaya ya Monduli,Joshua Nassari na kusema kuwa atakuja siku ya ijumaa desemba 14 mwaka huu kutoa maelekezo ya serikali.

Hata hivyo katika mkutano huo wa hadhara polisi Monduli wamemkamata mwenyekiti wa kijiji cha Kilimatinde,Merita Sangeti kwa tuhuma za uchochozi .

2 comments

Comments are closed.