MWENYEKITI wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Same, Azza Karisha amehitimisha mashindano ya Samia CUP yaliyokuwa yanachezwa kwenye tarafa Gonja jimbo la Same Mashariki michezo iliyoandaliwa na mbunge wa jimbo hilo, Anne Kilango.
Mashindano hayo yamehitimishwa kwa mchezo wa fainali uliokutanisha timu ya Ulimbo FC kutoka kata ya Mtii na Vuje FC kutoka kata Vuje ambapo timu ya Ulimbo FC iliibuka mshindi kwenye fainali hiyo na kutangazwa kuwa mabingwa wapya.
Pamoja na mambo mengine mwenyekiti huyo amemshukuru Anne Kilango kwa kuanzisha mashindano ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM akisema mashindano hayo yamekuwa na tija kubwa kwa vijana kwa maana ya kujenga umoja, upendo, mshikamano na kuimarisha afya zao.
“Niendelee kumshukuru na kumpongeza mwenyekiti wetu wa chama taifa ambaye ni Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.
Samia Suluhu Hassani na serikali yake kwa namna ambavyo amewajali wananchi wa tarafa ya Gonja na Kuwaletea fedha nyingi za Maendeleo kwenye sekta mbalimbali ikiwepo elimu, afya, barabara, kilimo nk”.
Alisema mwenyekiti huyo wa UVCCM Wilaya ya Same.
Pamoja na hayo amewaomba wananchi wa Gonja kuendelea kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassani na mbunge wa jimbo la Same Mashariki Anne Kilango na Chama Cha Mapinduzi.