Mwigulu aeleza azma ya Samia kukuza kilimo

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba amelieleza Bunge kwamba Rais Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuimarisha kilimo cha umwagiliaji na serikali ina fedha za kutekeleza miradi ya kilimo hicho.

Dk Mwigulu amesema bungeni Dodoma juzi wakati wa kuchangia hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka wa fedha 2023/24.

“Kw jinsi Mheshimiwa Rais alivyodhamiria kwenye jambo hilo la umwagiliaji hatujakosa fedha ya kutekeleza miradi ya umwagiliaji, hii ni awamu ya kwanza, tutaendelea na awamu nyingine na bajeti ya miradi mingine mikubwa tamko la kisera na bajeti,” alisema Dk Mwigulu.

Aliongeza, ulipaji wa miradi mikubwa ikiwemo ya barabara na ya kilimo ni wa hatua kwa hatua kulingana na ngazi ya utekelezaji. Hatuwezi kumlipa fedha zote mkandarasi siku moja. Hivyo hakuna fedha ambayo ina ukakasi kwenye utekelezaji wa umwagiliaji, na ni taratibu wa utekelezaji miradi ya kielelezo, na tumedhamiria kwenye miradi ya umwagiliaji.”

Dk Mwigulu alisema serikali ina mpango wa kuendelea kuiwezesha Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) kwa kuwa ni injini ya utekelezaji wa hatua ya Rais Samia kukifanya kilimo kiwe biashara.

Kuhusu utambuzi wa maeneo kwa ajili ya kilimo, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Angeline Mabula alisema hekta 2,216,076 zimetengwa kwa kilimo kutoka vijiji 1,059 kati ya vijiji 2,765 ambavyo vimewekewa mpango bora wa matumizi ya ardhi.

Dk Mabula alisema pia serikali imepima mashamba na kutoa hati za miliki ambazo hati 1,318 za kimila ambazo zimetumika kukopa takribani Sh bilioni 60 kutoka halmashauri 10.

Naibu Waziri wa Kilimo, Anthony Mavunde alisema wizara hiyo imeingia mikataba ya upembuzi yakinifu usanifu wa kina kwa mabonde 22 kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji zaidi ya hekta 300,000.

Mavunde alisema pia katika mwaka wa fedha 2022/2023, wamechimba mabwawa 14 yatakayozalisha lita bilioni 131 na kwenye mwaka wa fedha 2023/2024 yatachimbwa mabwawa mapya 100 yatakayozalisha lita 900 na vitachimbwa visima 150 kwenye halmashauri 184.

Habari Zifananazo

Back to top button