Mwigulu awananga wanasiasa

Asema kodi si zake wala za Rais Samia

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Mwigulu Nchemba  amewatolea uvivu wanasiasa ambao wamekuwa wakidai kuwa kodi zinazotozwa ni zake na Rais Samia Suluhu Hassan.

Akiwasilisha Bajeti Kuu ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 Bungeni Jijini Dodoma leo Juni 15,2023 Mwigulu amesema kodi zinatozwa ni za nchi na wala sio zake wala za Rais Samia na sio pia za TRA.

“Kumezuka dhana ya kuona kuwa kodi zinazotozwa ni kubwa bila kujali mzigo mkubwa wa Serikali kwa nchi yetu katika kugharamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo na utoaji wa huduma za jamii, kuna baadhi ya Wanasiasa wanasema kodi hizi ni za Samia, kodi hizi za Mwigulu, kodi hizi za TRA.

“Kodi zote zinazokusanywa huwekwa kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali uliopo Benki Kuu ya Tanzania, na baadae kupelekwa kwenye Wizara za Kisekta, fedha hizo ndizo zinazotumika kugharamia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo iliyopo mijini na vijijini.

“Ndio zinazotekeleza miradi ya umeme, maji, barabara, madaraja, vivuko, reli, usafiri wa anga, madarasa, zahanati, ununuzi na usambazaji wa dawa na malipo ya mishahara ya Watumishi kama Walimu, Wauguzi na Madaktari.

“Kila mmoja wetu ajue kuwa, Kodi sio jambo la Rais, kodi sio jambo la Waziri wa Fedha, kodi sio jambo la TRA, kodi ni jambo la nchi, kodi ndio maendeleo ya nchi yetu.

Amesema, kila mtanzania mwenye sifa za kulipa kodi ana wajibu wa kulipa kodi stahiki na halali kwa mujibu wa sheria, ni lazima kulipa kodi, ni lazima kutumika  mashine za EFD bila udhuru wowote, ni lazima kila anayeuza atoe risiti na anayenunua adai risiti

Habari Zifananazo

Back to top button