WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba amesema wizara hiyo imepokea maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuhusu kushughulikia malalamiko ya wananchi yaliyojitokeza kuhusu gharama za tozo za miamala ya kielektroniki.
Dk Mwigulu alisema hayo jana kwa nyakati tofauti wilayani Tarime mkoani Mara alipofanya ziara ya kikazi ya kutembelea mpaka wa Tanzania na Kenya katika mji wa Sirari na kuzungumza na wananchi, wafanyabiashara na wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Alisema wataalamu wa wizara hiyo wanayafanyia kazi maelekezo yaliyotolewa na Rais Samia, CCM na maoni ya wananchi kuhusu jambo hilo na akasema muda si mrefu serikali itakuja na majawabu baada ya kufanya marekebisho kadhaa ili kuleta unafuu.
Dk Mwigulu alisema nia ya serikali ni kukusanya mapato kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa kuweka miundombinu wezeshi inayolenga kuibua wajasiriamali wadogo, wa kati na wakubwa na hatimaye kuinua kipato cha mwananchi mmoja mmoja.
“Baada ya kupokea maelekezo ya Mheshimiwa Rais kuhusu kuyazingatia maoni ya wananchi yanayoendelea kutolewa, tunalifanyia kazi suala hilo na punde tutaleta majawabu,” alisema.
Dk Mwigulu alisema serikali inahitaji fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya kimkakati na mingine ya huduma za jamii ambayo pia inahitaji fedha.
Aliitaja baadhi ya miradi ambayo haiwezi kusimama kwa kukosa fedha ikiwemo ujenzi wa bwawa la kuzalisha umeme la Mwalimu Julius Nyerere unaogharimu zaidi ya shilingi trilioni 6, mradi wa reli ya kisasa-SGR unaogharimu zaidi ya Sh trilioni 23.
Dk Mwigulu aliitaja mingine kuwa ni upanuzi wa bandari, miradi ya Tarura, ujenzi wa hospitali na vituo vya afya, mradi wa elimu bila malipo, ujenzi wa vyumba vya madarasa, mabweni na nyumba za walimu na ujenzi wa vyuo vya ufundi.
Aidha, alisema shughuli zingine ambazo haziwezi kusimama ni ulipaji wa mishahara kwa watumishi, kugharamia miradi ya kilimo ukiwemo utoaji ruzuku kwenye mbolea, utoaji wa ruzuku ya mafuta ili kukabili mfumuko wa bei na miradi mingine inayoendelea kutekelezwa nchini.
Alitoa mfano wa baadhi ya miradi inayokusudiwa kutumia fedha zitakazopatikana kwenye tozo kuwa ni ujenzi wa vyumba vya madarasa elfu 17 kabla ya Januari mwakani na ujenzi wa vyuo vya ufundi-VETA katika wilaya 72 ambazo hazina vyuo hivyo ambapo jumla ya Sh bilioni 200 zitatumika kuvijenga.