Mwinyi ndiye alianzisha neno unyanyapaa

DAR ES SALAAM: Hayati Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili Ali Hassan Mwinyi ndiye mwanzilishi wa neno unyanyapaa.

Mzee Mwinyi ambaye hadi umauti unamfika Februari 29, 2024 kutokana na saratani ya mapafu, alikuwa Mkuu wa Chuo cha Afya cha Sayansi Shirikishi (Muhas).

Akizungumza katika uzinduzi wa Afua ya Mfumo Jumuishi kwa Watoa Huduma za Afya ili kupunguza unyanyapaa kwa watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi na watumiaji wa dawa za kulevya, Mhadhiri na Mtafiti wa Muhas, Dk Jessie Mbwambo amesema hayati Mzee Mwinyi ndiye mwanzilishi wa neno unyanyapaa.

“Mwaka 2003 tarehe kama ya leo tulizindua utafiti wa kupinga wanaotengwa kutokana na maradhi ya Ukimwi, utafiti huo ndio ulizaa tafiti nyingi za unyanyapaa. ikiwemo hii ya Afua Jumuishi kwa watoa huduma.

“Wakati tunazindua utafiti huo Mzee Mwinyi akatuambia kwa nini tusiwe na jina zuri ambalo litaingizwa kwenye kamusi yetu ya Kiswahili, akaja na neno Nyenyepa….

“Lakini katika kulichakata likaonekana lugha haijakaa sawa sawa ndio likazaliwa neno Nyanyapaa linalotumika mpaka leo,”amesema Dk Mbwambo.

Amesema neno hilo lilikuja kutokana na matendo yaliyokuwa yakiendelea katika jamii ya kuwatenga wagonjwa wa ukimwi na watumiaji wa dawa za kulevya na neno hilo unyanyapaa likaanza kutumika rasmi Machi 1, 2023 ikiwa ni siku ya kupinga unyanyapaa duniani na leo likiwa limetimiza miaka 20 tangu kuasisiwa kwake.

Habari Zifananazo

Back to top button