Mwitikio chanjo ya Uviko 19 waongezeka Mpanda

IDADI ya watu wanaojitokeza kupata chanjo kwenye vituo mbalimbali vinanyotoa huduma za chanjo ya Uviko 19 imeongezeka kutokana na hamasa kubwa inayotolewa na Serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali ikiwemo taasisi ya TAYOBECO.

Hayo yamebainika katika kikao cha tathmini ya utekelezaji wa mradi wa Boresha Habari unaotekelezwa katika Manispaa ya Mpanda na taasisi ya Tanzania Youths Behavioural Change Organization (TAYOBECO) tokea ulipoanza mwezi Februari mwaka huu, kikao kilichowashirikisha watoa huduma za afya ngazi ya jamii na wadau mbalimbali wa afya.

Imebainika kuwa hamasa hiyo imefanya watu kuona umuhimu wa chanjo ya hiyo pamoja na chanjo za aina nyingine ikiwemo surua.

Akizungumza Mratibu Msaidizi wa chanjo Manispaa ya Mpanda Patrick Kumburu, wakati wa kikao hicho amesema kuwa idadi ya watu wanaojitokeza kwenye vituo vya kutolea chanjo ya Uviko 19 imeongezeka kufuatia wananchi kupata uelewa kutokana na mradi huo.

Kumburu amefafanua kuwa vyombo vya habari vimesaidia pia kuwafanya wananchi watambue umuhimu wa huduma ya chanjo ya Uviko 19,  lakini pia hata magonjwa mengine ya mlipuko wa janga la surua lililokuwa limeukumba Mkoa wa Katavi.

Amesema watoa huduma za afya ngazi ya jamii, hawakuhangaika sana kuwafikia wananchi na kuweza kupata uelewa moja kwa moja juu ya umuhimu wa huduma za chanjo mbalimbali, ambazo zimekuwa zikitolewa kwenye vituo vya kutolea chanjo.

“Chanjo ya Uviko 19 hapo awali  vituo ambavyo vilikuwa vinatoa huduma havifiki kumi, vituo vingine vilikuwa vinasuasua, watu walikuwa na dhana potofu juu ya huduma hizi za chanjo, lakini kutokana na mradi wa TAYOBECO umesaidia sana kuongeza nguvu ya uelewa kwenye jamii na ndiyo maana leo tuna vituo 28 ambavyo vinaripoti huduma za UVIKO 19,” amesema.

Mratibu wa mradi wa Boresha Habari wa taasisi ya TAYOBECO, Adinani Mussa, amesema kuwa wamekuwa wakifanya kazi na Shirika la Internews Tanzania, na kwa zaidi ya miaka mitatu sasa shirika hilo limekuwa likitekeleza  mradi huo unaofadhiliwa na USAID.

Amesema lengo la mradi huo ni kuhamasisha vijana, wanawake na makundi mengine mbalimbali wakiwemo wazee juu ya umuhimu wa chanjo ya Uviko 19 pamoja na chanjo nyingine kama surua.

Amebainisha kuwa kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa hivi karibuni Mkoa wa Katavi ni miongoni mwa mikoa ambayo ilikuwa na mwitikio mdogo wa chanjo ya uviko 19 na ndio maana wakaona mradi huo kuupeleka Manispaa ya Mpanda.

Mtoa huduma za afya ngazi ya Jamii katika Kata ya Mpanda Hotel, kwenye kituo cha Afya Mwangaza, Jolard Makori amesema ameweza kuhamasisha watu 441 ambao wamekubali kuchanja chanjo ya Uviko 19, ambapo hapo awali katika kituo hicho waliojitokeza hawakuzidi watu 100.

Kwa upande wake Neema Hussein mkazi wa Mtaa wa Mjimwema Manispaa ya Mpanda amesema amehamasika kuchanja baada ya kusikia matangazo mbalimbali kupitia vyombo vya habari yaliyokuwa yakitokewa na taasisi ya TAYOBECO.

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x