Mwitikio mkubwa Dodoma tiketi za mabasi mtandaoni

MAMLAKA ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), imesema kuna mwitikio mkubwa mkoani Dodoma wa wananchi kukata tiketi kielektroniki kwa mabasi yaendayo mikoani

Hatua hiyo imekuja huku mamlaka hiyo ikisisitiza kuwa mabasi yote yaendayo mikoani, ambayo yatakuwa hayajajiunga na mfumo wa tiketi mtandao yatasimamishwa kufanya shughuli za usafirishaji kuanzia Alhamii wiki hii.

Ofisa Uhusiano Mwandamizi wa LATRA, Salum Pazzy amesema hayo alipokuwa akizungumza na HabariLeo, kuhusu ukaguzi wanaoendelea kuufanya katika mikoa mbalimbali na kubaini changamoto zinazowakabili abiria kutokana na baadhi ya mabasi kukaidi agizo hilo.

Amesema kwa stendi ya Dodoma muitikio wa mabasi wa kutumia teknolojia hiyo  ni asilimia 95, isipokuwa kwa kampuni moja walibaini kuna tatizo, waliizuia kwa muda na kutoa onyo.

Pazzy amesema baada ya serikali kuagiza mabasi yajiunge na mfumo huo, iliongeza muda wa ziada kwa miezi miwili kuanzia Julai mosi hadi Agosti 31, ambao unaisha Jumatano, hivyo baada ya hapo hatua za kinidhamu zitachukuliwa.

Amesema Septamba mosi, LATRA itaanza kutoa adhabu ya faini ya Sh 250,000 kwa mmiliki atakayekiri kosa, lakini asipokiri kosa na kufikishwa mahakamani kisha akaonekana ana kosa sh 500,000 au kifungo cha miezi sita jela, ama adhabu zote kwa pamoja.

Amesema Latra imekuwa ikiendelea kutoa elimu ya mfumo huo tokea April mwaka huu kwa kuzunguka nchi nzima, ili wananchi pamoja na wamiliki waelewe faida ya teknolojia hiyo.

“Siku chache zilizopita tulikuwa stendi ya Mwanza na leo tupo stendi Kuu ya mabasi Dodoma kwa ajili ya kufuatilia jambo hili.

“Tukiwa Mwanza tumekuta abiria zaidi ya 100 wametapeliwa wamenunua tiketi sio za kieletroniki kwa mabasi mawili, mwisho wa siku mkataji wa tiketi hizo alipatikana, lakini abiria walikuwa wameshapata usumbufu mkubwa,” amesema.

 

Habari Zifananazo

Back to top button