Mwitikio mkubwa shule zikifunguliwa

SHULE za awali, msingi na sekondari zimefunguliwa huku wanafunzi wengi wakionekana kuitikia mwito wa kujiunga na shule za serikali.

Pamoja na wazazi na walezi kuitikia mwito wa serikali wa kupeleka watoto shule, imeonekana maagizo yote ya serikali yametekelezwa ikiwamo wasio na sare kupokelewa na wanafunzi wote kukaa kwenye madarasa.

Sambamba na hayo wanafunzi wa Shule ya Msingi Jorodomu na sekondari Ganana katika Halmashauri ya Wilaya ya Hanang, jana walianza siku kwa maombolezo baada ya kuripoti shule na kugundua baadhi ya wanafunzi wenzao walikufa kwenye maporomoko ya matope mwishoni mwa mwaka jana.

Advertisement

Jumla ya watu 89 walikufa na 139 kujeruhiwa katika maporomoko hayo yaliyosababishwa na kupasuka kwa miamba ya mlima Hanang.

Baadhi ya wanafunzi na walimu walishindwa kujizuia na kutokwa na machozi baada ya kubaini wenzao wengine hawataonana tena baada ya kusikia walikufa kwenye maafa hayo.

Katika Shule ya Msingi Jorodomu walifariki wanafunzi 15 huku Shule ya Sekondari Ganana walifariki wanafunzi wawili.

Maafa hayo yalitokea Desemba mwaka jana ambapo watu 89 walipoteza maisha na 139 kujeruhiwa.

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga ametoa siku tatu kuanzia leo kwa maofisa elimu wa shule za msingi na sekondari kuhakikisha wanafunzi wote wanarejea shuleni hasa wale ambao hawajaathiriwa na tukio la mafuriko.

Arusha

Kwa ujumla, wanafunzi 32,000 wa darasa la kwanza wameanza masomo katika Halmashauri ya Jiji la Arusha katika mwaka wa masomo 2024/25 idadi ambayo ni kubwa na imevunja rekodi kwani haijawahi kutokea kwa kipindi kirefu.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, Juma Hamsini alisema kuwa shule zote katika Jiji hilo zimefunguliwa kwa ajili ya kuanza muhula mpya wa masomo.

“Hadi Januari 5, mwaka huu wanafunzi wanaojiunga na masomo ya kidato cha kwanza katika shule zetu za sekondari zilizo ndani ya Jiji la Arusha ni wanafunzi 14,471, wanafunzi walioandikishwa kujiunga na shule za msingi darasa la kwanza ni wanafunzi 11,521 na wanafunzi waliyoandikishwa kujiunga na masomo ya awali ni 8,160,” alisema.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella ametoa siku tatu kwa uongozi wa Jiji la Arusha kuhakikisha wanajenga uzio utakaotenganisha madarasa ya awali ya Shule ya Msingi Murriet Darajani, lakini pia umaliziaji madarasa mawili ili kupunguza msongamano wa wanafunzi wa madarasa ya awali.

Aidha, aliagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuchunguza Shule ya Sekondari ya Mlimani Murriet ambayo awali gharama zake za ujenzi zilikuwa juu kuliko uhalisia wa shule yenyewe huku saruji, rangi na miundombinu yake ikiwa hairidhishi.

Mongella aliiagiza Takukuru kuchunguza gharama za madawati ya shule hiyo pamoja na miundombinu iliyogharimu Sh bilioni 1.1.

Pia Mongella aliagiza vifaa vya michezo kwenye madarasa ya awali viwekwe na uzio unaotenganisha kati ya madarasa ya awali na msingi ambao utasaidia wanafunzi hao kutopotea au kuchangamana na watoto wengine wakubwa.

Shinyanga

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Christina Mndeme ameagiza kuendelea kutafutwa kwa mzazi anayeishi Kata ya Lyamidati aliyekimbia baada ya kuchukua ng’ombe 15 kwa ajili ya kumuozesha mtoto wake wa kike aliyefaulu na kuchaguliwa kuingia kidato cha kwanza.

Tukio la kumuozesha mwanafunzi limetokea juzi na baadhi ya wananchi waliokerwa na kitendo hicho walitoa taarifa hiyo kwa siri na mzazi alipovamiwa kwa kutaka kukamatwa alitoroka.

Mndeme alisema hayo jana alipokuwa akitembelea shule mbalimbali kujionea kuripoti kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Ngokolo na shule mpya ya sekondari ya wasichana ya Shinyanga huku akiwataka wazazi kuacha tabia hiyo mara moja.

“Mtoto aliyefaulu alipata wastani wa A tumemchukua na kumpeleka shule aliyopangiwa na kuhakikisha serikali inamsimamia na kuendelea na masomo yake,” alisema.

Pwani

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge amewataka walimu wakuu kutowarudisha nyumbani wanafunzi ambao wameripoti shuleni na wana upungufu wa baadhi ya vifaa kama sare.

“Nimeridhishwa na mapokezi ya wanafunzi wa kidato cha kwanza na darasa la kwanza tunaamini wanafunzi watasoma kwenye mazingira mazuri, serikali imeboresha mazingira ya usomaji,” alisema.

Alieleza kuwa mkoa unatarajia kupokea wanafunzi 55,771 darasa la awali, 51,446 darasa la kwanza na 40,796 kidato cha kwanza.

Dar es Salaam

Idadi kubwa ya wanafunzi imejitokeza kuanza masomo ya awali, msingi na sekondari katika shule mpya za serikali zilizojengwa katika Wilaya ya Ubungo mkoani Dar es Salaam.

Hilo limebainika katika ziara iliyofanywa na Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Hashim Komba katika shule mbili ikiwemo Shule ya Sekondari Wasichana Dar es Salaam iliyoko Kwembe na Shule ya Msingi Goba Mpakani.

Mkuu wa Sekondari ya Wasichana ya Dar es Salaam, Elizabeth Bonzo alisema katika shule hiyo mpya ya sayansi tayari wanafunzi 103 kati ya 215 waliotakiwa kuripoti, wamesharipoti shuleni hapo.

Mkuu wa wilaya hiyo, Komba alisema shule hiyo ni miongoni mwa shule 10 za sayansi nchi nzima zilizojengwa na serikali kwa ajili ya kumwezesha mtoto wa kike kwenye masomo ya sayansi.

Kwa upande wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mohamed Mchengerwa ametaka kuwe na uwiano sawa wa walimu na wanafunzi katika shule.

Mchengerwa aliyasema hayo jana alipofanya ziara ya kukagua mapokezi ya wanafunzi wa kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari ya Benjamin Mkapa mkoani Dar es Salaam.

Alisema kupitia utaratibu wa viongozi kupita shuleni kupokea wanafunzi wa awali, darasa la kwanza na kidato cha kwanza wamebaini mlundikano wa walimu kwenye baadhi ya shule huku kukiwa na walimu wachache kwenye shule zingine.

“Sasa namuelekeza Katibu Mkuu anayeshughulikia Elimu Tamisemi (Charles Msonde) kufanya msawazo wa walimu nchi nzima ili kuwe na uwiano sawa wa walimu na wanafunzi katika shule zote. Sio shule ina wanafunzi wachache lakini ina walimu wengi ili hali shule zingine zikiwa na walimu wachache na kuwa na wanafunzi wengi,” alisema.

Tanga

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Waziri Kindamba ameonya viongozi wa shule za msingi na sekondari kutowachangisha wazazi nje ya utaratibu utakaotokana na vibali kutoka ofisi yake kwa vile gharama za masomo zimeshalipwa na serikali.

Alisema kama kuna utaratibu wa michango ni lazima kuwepo na kibali kutoka kwenye ofisi ya mkuu wa mkoa kinachoonesha ruhusa na sababu ya michango hiyo bila hivyo hakuna mzazi kuchangishwa fedha yoyote.

Shule nane mpya zilizojengwa kwa Mradi wa Kuboresha Elimu ya Sekondari (SEQUIP) mkoani Geita zipo tayari kwa ajili ya kuanza kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza kwa mwaka mpya wa masomo.

Ofisa Elimu Sekondari Mkoa wa Geita, Anthony Mtweve alisema shule zote nane zimeshakamilika kwa zaidi ya asilimia 90 ambapo kati yake shule saba ni shule za kata huku shule moja ni shule yenye hadhi ya mkoa inayojengwa mjini Geita.

“Utoshelevu wa vyumba vya madarasa, kwa madarasa yote yanatosha, sema tu kwamba havitatosha kwa wastani wa wanafunzi 45, badala yake tumeongeza mpaka wastani wa wanafunzi 50 kwa darasa,” alisema.

Alisema mkoa unategemea kupokea jumla ya wanafunzi 52,568 wa kidato cha kwanza waliofaulu mtihani wa darasa la saba kwa mwaka 2023.

Morogoro

Maelfu ya wanafunzi wa shule za sekondari na shule za msingi katika Manispaa ya Morogoro wameripoti shuleni siku ya kwanza na kuandikishwa kuanza muhula wa masomo wa mwaka 2024.

Katika Shule ya Sekondari Morogoro, Mkuu wa Wilaya, Rebeca Nsemwa aliwataka wasome kwa bidii ili wafaulu na kuendelea kidato cha tano na sita hadi kufika elimu ya juu.

Mtwara

Baadhi ya wazazi katika Kata ya Magomeni Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara wameipongeza serikali kwa kuwajengea miundombinu ya shule kwenye maeneo yao.

Mkazi wa Magomeni Kagera katika manispaa hiyo, Hadija Hamisi alisema serikali imekuwa na jitihada kubwa kuhakikisha watoto wanasoma katika mazingira yaliyokuwa rafiki huku akiahidi kutoa ushirikiano kwa kuhakikisha mtoto anaripoti shuleni hapo bila kukosa.