Mwongozo kuwalipa walimu posho saa za ziada waandaliwa

NAIBU Waziri, Ofisi ya Rais-Tamisemi, Deogratias Ndejembi amesema serikali haina posho ya mazingira magumu kwa walimu lakini iko katika maandalizi ya mwongozo wa ulipaji posho ya saa ya ziada.

Aidha, amewaagiza Makatibu Tawala wa Mikoa ya Tanzania Bara kufanya msawazo wa walimu kutoka shule zenye ziada na kuwapeleka katika shule zenye upungufu zaidi.

Ndejembi alisema hayo jana bungeni wakati wa kujibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu, Kunti Majala (Chadema).

Katika swali lake, Majala alitaka kujua ni lini serikali itatoa posho ya mazingira magumu kwa walimu walio vijijini hususani wanawake.

Akijibu swali hilo, Ndejembi alisema serikali inaweka uwezeshaji kwa walimu kwa kujenga nyumba karibu na shule. Alisema hakuna posho mahususi ya mazingira magumu.

“Kwa sasa tunaendelea na kazi ya kuandaa mwongozo wa ulipaji posho kwa saa za ziada,” alisema.

Katika swali la nyongeza, Majala alitaka kujua mpango wa serikali wa kupeleka walimu wa kike katika shule za sekondari na msingi wilayani Chemba.

Akijibu swali hilo, Ndejembi alisema serikali imekuwa ikitoa ajira kukabiliana na upungufu wa walimu shuleni unaotokana na walimu kustaafu, kuacha kazi, kufukuzwa, kufariki na ongezeko la idadi ya wanafunzi wanaoandikishwa.

Alisema kwa mwaka 2021/22, serikali imeajiri walimu 26,598 wakiwamo 16,640 wa shule za msingi na 9,958 wa shule za sekondari.

Alisema kwa upande wa ajira zilizotangazwa mwaka 2021/22, Halmashauri ya Wilaya ya Chemba ilipata walimu 46 wa kiume na walimu 49 wa kike kwa shule za msingi na sekondari.

“Ofisi ya Rais-Tamisemi imetoa maelekezo kwa makatibu tawala wa mikoa wote Tanzania Bara kufanya msawazo wa walimu kutoka shule zenye ziada na kuwapeleka katika shule zenye upungufu zaidi kwa kuzingatia jinsia ili kuwa na uwiano wa walimu wa kike na kiume kwenye shule zetu mbalimbali,” alisema.

Habari Zifananazo

Back to top button