MWANAFUNZI raia wa Zambia ambaye alikuwa akitumikia kifungo nchini Urusi na kufariki akipigana na wanajeshi wa Urusi nchini Ukraine alikuwa ameajiriwa na kundi la mamluki la Urusi Wagner, kiongozi wake alisema.
Mkuu wa Kikundi cha Wagner Yevgeny Prigozhin amesema kwenye taarifa iliyonukuliwa na Shirika la Habari la AP kuwa mwanafunzi huyo, Lemekhane Nyireda mwenye umri wa miaka 23, “alifariki kishujaa.”
Waziri wa Mambo ya Nje wa Zambia Stanley Kakubo alisema mapema mwezi huu kwamba maafisa wa Urusi waliiarifu serikali ya Zambia kuhusu kifo cha Nyireda, ambaye alikuwa mwanafunzi aliyefadhiliwa na serikali kabla ya kuhukumiwa nchini Urusi kwa uhalifu ambao haukutajwa Aprili 2020.
Ubalozi wa Zambia katika mji mkuu wa Urusi wa Moscow ulibaini kuwa Nyirenda alifariki Septemba 22 na kwamba mabaki yake yalisafirishwa hadi mji wa mpakani wa Urusi wa Rostov kabla ya kurejeshwa Zambia.
Kabla ya kifungo chake jela, Nyirenda alikuwa akisomea uhandisi wa nyuklia katika Taasisi ya Fizikia ya Uhandisi ya Moscow. Alikuwa akitumikia kifungo chake cha takriban miaka tisa katika gereza lililo nje kidogo ya jiji la Moscow, serikali ya Zambia ilisema.