‘Mzazi aliyedai kuchapwa fimbo na mwalimu afungue kesi’

WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Doroth Gwajima amesema sakata la Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Kibweheri iliyoko Ubungo Dar es Salaam, Andrea Wanjala kudaiwa kumpiga fimbo mwanamke mfanyabiashara ndogondogo, Maisara Sirro ni udhalilishaji.

Gwajima amesema Maisara anapaswa kufungua kesi polisi, wizara yake itamsaidia.

Gwajima amesema hayo baada ya kutakiwa kutoa ufafanuzi juu ya tukio hilo lililotokea Februari 28 mwaka huu katika shule hiyo ya Kibweheri.

“Kifupi huu ni udhalilishaji anatakiwa afungue kesi polisi. Tutamsaidia,” amesema Gwajima.

Naye Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda amesema jambo hilo ni jinai, ambalo polisi wanapaswa kuchukua hatua.

“Hapana hii ni jinai, polisi wachukue hatua,” amesema Profesa Mkenda.

Akizungumzia tukio hilo, mwanamke huyo mwenye watoto wawili amesema, Februari 28 mwaka huu majira ya saa tano asubuhi alimpeleka shule mwanafunzi ambaye si mtoto wake aliyekuwa akizurura nje ya nyumba yake shuleni akielezea kuwa yeye ni mama mdogo wa mwanafunzi huyo.

“Nilimpeleka mtoto ambaye si wangu shuleni baada ya kumuona anazunguka zunguka jirani na nyumba yangu, mimi ninakaa karibu na shule nilipomuona mtoto huyo nilimuuliza kwa nini anazunguka haendi shule, akaniambia nimefukuzwa shule.

“Mtoto huyo anasoma kidato cha pili katika shule hiyo, hivyo ili asipoteze masomo nikampeleka na kusema mimi ni mama yake mdogo,” amesema.

Ameeleza baada ya siku chache mtoto huyo alisimamishwa tena masomo na kurudi nyumbani kwake, ili kuomba msaada, alipomuuliza amefanya nini mtoto huyo alimjibu kuwa amekutwa na mafuta ya Mwamposa.

Amemueleza kuwa kulikuwa na mwanafunzi amepandisha mashetani hivyo akampaka mafuta hayo.

Kwa maelezo ya mwanamke huyo alimchukua mwanafunzi huyo na kumpeleka tena shuleni kuieleza shule anajiondoa kwenye kumdhamini kwa kuwa sasa anaona mtoto huyo amekuwa na makosa ya mara kwa mara, asijekupata matatizo makubwa zaidi.

“Nilipokwenda mwalimu mkuu aliniuliza kwa nini nimempeleka mtoto ambaye si wangu na kusema kuwa ni mtoto wangu?

“Pale ofisini kwake alinichapa fimbo mbili, akagonga kengele watoto wakaenda mstarini nikachapwa mbele ya umati wa wanafunzi na walimu fimbo nyingine nne kwenye makalio,” alisema mwanamke huyo.

Amesema Mkuu huyo wa shule alimchapa na kusema kuwa anafanya hivyo ili iwe fundisho kwa wazazi wengine wenye tabia kama hizo.

Akizungumzia suala hilo, Mkuu huyo wa shule Wanjala ambaye anatuhumiwa kumchapa mwanamke huyo amesema mwanamke huyo hakuwa mzazi wa mwanafunzi huyo bali ni mtu alikwenda shuleni hapo mara mbili kwenye kikao akidanganya.

“Tulijiuliza, tulitaka kujua ana miadi gani na mtoto. Tukajiridhisha alikuwa na nia ovu na mtoto huyo. Akachagua adhabu aliyoitaka tunachofanya sasa ni kuhakikisha usalama kwa mwanafunzi,” amesema Wanjala.

Kuhusu kumchapa mwanamke huyo, Wanjala alipinga kwamba jambo hilo halikufanyika, hawezi kuelezea zaidi kwa kuwa lipo hatua ya juu.

Awali Mjumbe wa shina namba nane Kibwegere, Ephraim Vawunge amesema aliletewa hizo taarifa na hakuona haja ya kusubiri, hivyo alimwandikia barua mwanamke huyo aende serikali ya mtaa ili apate ruhusa aende polisi.

Kuhusu jambo hilo Ofisa Elimu Mkoa wa Dar es Salaam, Abdul Maulid amesema alifuatilia jambo hilo na kuambiwa Mkuu wa Wilaya ya Ubungo ameshalimaliza, hivyo hakuna haja ya kulifufua tena.

Habari Zifananazo

Back to top button