Mzee Jangala anavyopambana na Sanaa za maonesho

Msanii Mkongwe nchini, Mzee Jangala

“SISI wasanii wa kikundi cha Sanaa za Maonesho Mandela (Mandela Theatre Troupe), tumeona sanaa zetu za maonesho zinatoweka, tumeona kuna haja ya kuzifufua na kuziendeleza sanaa zetu zote za maonesho,” anasema  kiongozi wa kikundi hicho, Bakari Mbelemba ‘Mzee Jangala’ wakati wa mahojiano hivi karibuni kuhusu utamaduni na maana yake kwa taifa.

Kikundi hiki kilichoanzishwa mwaka 1984 na kupewa usajili na Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) wenye namba BST/049 ni moja ya vikundi vilivyovuma  kutokana na umahiri wake katika kuelimisha jamii masuala mbalimbali yanayohusu ustawi na ushiriki katika shughuli za uchumi.

Pia kimetumika katika kukemea vitendo viovu kwa hiyo wanapoona hali ya sasa ilivyo wanakuwa na nia ya kurejea tena ulingoni kuungana na serikali na jamii kukemea vitendo viovu ambavyo vimeshamiri kwenye jamii.

Advertisement

Kuwepo kwa vitendo vinavyoleta mmomonyoko wa maadili na uvunjifu wa amani hapa nchini, kwa kuzingatia madhumuni ya kuanzishwa kwake, Mzee Jangala anasema wanataka kurejea kivingine kwa ajili ya manufaa ya nchi na manufaa ya vizazi vya sasa.

Wakiwa wametembelea mikoa yote nchini kwa masuala mbalimbali ya kijamii na kufanya ziara katika nchi za Sweden, Denmark, Finland, Ujerumani, Nigeria, Zimbabwe, Kenya na Uganda, Mzee Jangala anasema wanajua ambacho kwa sasa hakipo na kinazidi kuiondoa Tanzania katika utamaduni wake, mifumo ya kujifunza na kurithisha haipo.

“Tumekaa na kuona kwamba tuombe mkopo kama wajasiriamali katika Mfuko wa Utamaduni ili tupate vyombo vya muziki vyenye ubora na vyombo vya kuzalishia kazi za filamu na tamthilia zenye maudhui ya nchi yetu,” anasema Mzee Jangala.

Kikundi hicho kimefanya kazi na Watanzania na watu wa nje kama Wizara ya Afya, Benki ya Dunia, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Mamlaka ya Chakula na Dawa (TDFA) na Taasisi ya chakula na lishe.

Mzee Jangala anaamini kwamba Mfuko wa Utamaduni unaweza kusaidia wajasiriamali wanaojua nini wanakifanya kwa kuangalia machapisho yao (miradi) na kuipitisha ili si tu kutengeneza faida bali kuhifadhi utamaduni.

Utamaduni ambao ama hakika ni kielelezo cha utaifa, huenda ukahitaji utashi wa mtu binafsi kuwezesha kuutunza kuliko sheria kwani baadhi ya kazi ambazo zinatafutwa kufanyiwa kazi zinaweza zikatunza utamaduni kwa ajili ya utalii na vizazi vijavyo lakini visitengeneze faida ya moja kwa moja katika biashara, anasema Mzee Jangala.

Mathalani utengenezaji wa ngoma, uwambaji wa ngoma, utengenezaji wa marimba matumizi yake ni mambo ambayo huyategemei kuuzika siku hiyo lakini kwa kuingiza katika kituo cha utamaduni, watu wakaelimishwa inakuwa ni sehemu ya utalii.

Mzee Jangala anasema kikundi kimeandika mradi mkubwa ambao pia utawapatia nafasi ya kuzalisha na kuuza kazi za sanaa na utamaduni kwa kutumia wasanii wa ndani ya kikundi na wengine watakaoalikwa kwa lengo la kubadilishana utaalamu sanaa za jukwaani hapa nchini.

“Mimi na wenzangu tunataka kutafsiri ndoto ya kufufua, kukuza na kudumisha sanaa zetu zote hapa nchini kwa kuzingatia maadili na maudhui ya nchi yetu, tunaamini mfuko wa utamaduni utaliwezesha hili,” anasema.

Wazo la Mzee Jangala na kikundi chake kuhusu utamaduni kwa kuwa na kituo ambacho mafunzo yanaanzia katika ubunifu na uumbaji wa vifaa vya asili vya mwanzo wa utamaduni (ngoma) na hata marimba, linaweza kusaidia kutunza utamaduni kama yalivyo mataifa mengine yaliyoendelea kama China na nchi za Scandinavia ambazo zina vituo na  vikundi vya kitaifa vya ngoma na muziki wa kwao.

Pamoja na ushindani uliopo katika sanaa, tatizo kubwa lililopo sasa, ni kuvurugika kwa sanaa ya asili kama ngoma za asili za makabila mbalimbali, maigizo, sarakasi, muziki wa dansi na taarabu ya asili.

“Tumeandika mradi huu, kutokana na uzoefu wetu, soko lipo na hatuna shida na ubunifu, uasili na upelekaji wa ujumbe kwa jamii, shida yetu tunaeleweka kwa watu wanaotakiwa kutusaidia?

,” aliuliza Jangala ambaye alidokeza kwamba pamoja na kuwepo kwa mradi huo anapoulizwa ulipaji wake wa kodi na uhai wa akaunti ya benki kuingiza na kutoa anaona kuna mkwamo katika kuangalia utamaduni katika upana wake na kwa nini Rais Samia Suluhu Hassan aliagiza kurejeshwa kwa mfuko huo.

“Naamini kwamba mama (Rais Samia) ameona shida ya kuhifadhi utamaduni na kuendeleza sanaa kuwa na faida kwa uhai wa taifa na pia kwa uhai wa kiuchumi. Lakini najiuliza kama watendaji wanaelewa. Naulizwa swali la toka kikundi kianze kuhusu ulipaji kodi, unamweleza mtu zamani mlifanyaje bado hakuelewi na wala hakusaidii wewe kuelewa. Mfuko huu ninavyofikiri kwa jina tu ni pamoja na kuhifadhi utamaduni na hili si jambo rahisi kama kutoa mikopo. Ni vyema wataalamu wakasoma hii miradi na kuiangalia faida yake kwa taifa,” anasema.

Anasema mradi huo kwa umri wake ulikuwa wa kuweka sawa mambo ambayo amekuwa akishiriki nayo akiwa mwalimu wa Sanaa Bagamoyo, Mtumishi wa serikali na pia msanii ambaye ameshafanyakazi ndani na nje ya nchi na kushiriki katika kikundi cha taifa cha sarakasi na maigizo.

“Hatuna vikundi vya taifa vya ngoma, maigizo wala sarakasi, vikundi hivi ambavyo havipo kwa sasa vilikuwa ni vikundi vya kuweka uhai wa utamaduni na pia kuhifadhi, nimeyaona hayo na umuhimu wake nataka kurejesha yaliyo muhimu katika mlolongo wa utamaduni kama uhai wa taifa,” anasema Jangala.

Katika mahojiano alinionesha mradi wenyewe ukiwa umechanganuliwa vyema na unaweza kuanza kulipwa miezi saba baada ya kuanza kutekelezwa.

“Kwangu mimi mwandishi naona mradi huu utasaidia kukuza vipaji vya wasanii hasa vijana kwa kuwapatia elimu ya kutosha kuhusu vifaa mbalimbali vinavyotumika katika kuuenzi utamaduni, kwa mzee wa miaka 70 akiwa na tuzo ya Zeze iliyotolewa na  mfuko wa utamaduni  mwaka 2002 kwa kutambua na kuenzi mchango wake uliotia fora katika maendeleo ya utamaduni kwenye eneo la sanaa za maonesho ni vyema kuona nia njema na kuisaidia kutimia.”

Rais wa Benki ya Dunia, Paul Wolfoeitz  Agosti 8, 2006 alimwandikia barua Mzee Jangala akimwelezea anavyoheshimu kazi ya kikundi cha Mandela katika kuhamasisha maendeleo na ustawi wa taifa la Tanzania na kusema wao ni washirika wa kweli wa maendeleo ya Tanzania.

Naam washirika wa maendeleo ya Tanzania wanaona kazi inayofanywa na kikundi hiki chini ya Mzee Jangala Mfuko wa Utamaduni mkaribisheni ofisini kwenu mshauriane nini kifanyike maana mmomonyoko wa maadili umefika pabaya.

1 comments

Comments are closed.

/* */