Mzumbe waandaa tamasha kuibua vipaji

CHUO Kikuu Mzumbe kilichopo mkoani Morogoro kimeandaa tamasha ‘Mzumbe Day’ lenye lengo la kuibua vipaji na mawazo bunifu ya wanafunzi wa chuo hicho.

Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Ubunifu Ujasiriamali na Mahusiano ya Kitasnia ya Chuo Kikuu hicho ,Dk Emmanuel Chao alisema hayo mjini Morogoro, ambapo alisema hatua hiyo inalenga kuwajengea uwezo wa kujiajiri ili kupunguza changamoto ya ajira.

Dk Chao alisema kambi hiyo itashirikisha wanafunzi wa chuo hicho, wahitimu wa chuo wa ndani na nje pamoja na wadau mballimbali kwa ajili ya kuonesha ubunifu wa kazi zao.

Tamasha hilo litabeba kauli mbiu ya “ Kukumbatia Teknolojia zinazoibukia na mbinu mpya za kujifunza kwa ajili ya maendeleo endelevu” na lengo ni kuwawezesha vijana kukabiliana na changamoto za upatikanaji wa soko la ajira nchini hususani kwa wanaohitimu chuo hicho.

Dk Chao alisema kambi hiyo inatarajia kuanza Machi 20 na kufikia tamati Machi 22 , ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Nchi ,Ofisi ya Waziri Mkuu , Kazi , Vijana , Ajira na Wenye Ulemavu , Profesa Joyce Ndalichako.

“Chuo chetu hii si mara ya kwanza kufanya tukio hili, tumeaanza mwaka 2017 kwa kuandaa kambi za ujasiriamali kwa ajili kuibua vijaji na mawazo bunifu kwa ajili ya kuisaidia jamii,“ alisema Dk Chao.

Alitaja mambo mambo mengine yatakayofanyika ni bonaza la michezo mbalimbali ikiwemo riadha itakayowashirikisha wanafunzi, walimu na wadau mbalimbali ,mafunzo ya elimu ya afya kwa jamii na maonesho ya bidhaa za ubunifu.

Dk Chao alisema Profesa Ndalichako atashiriki siku ya pili kwa kuhudhuria ushindanishaji mawazo ubunifu ya wanafunzi wa chuo hicho na kasha kutoa zawadi kwa washindi watatu watakao shinda mawazo bunifu kutoka kwa miongoni mwa washiriki kadhaa.

Alisema siku ya tatu tamasha hilo kutatolewa mafunzo mbalimbali ya ujasiriamali na ubunifu yatakayowahusisha na kuwakutanisha wanafunzi wa chuo hicho ,walimu na wadau mbalimbali .

“ Wanafunzi watanufaika na mafunzo ambayo walikuwa hawayapati darasani , sasa watayapata kutoka kwenye makampuni na Mashirika mbalimbali likiwemo la Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO).

Habari Zifananazo

Back to top button