MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, ameushauri uongozi wa Chuo Kikuu Mzumbe (MU),kuanzishwa kwa mfuko wa ufadhili wa wahitimu wa Chuo Kikuu hicho “ Alumni Scholarship Scheme” .
Uazishwaji wa mfuko huo utawasaidia Watanzania ambao wana sifa ya kusoma katika ngazi ya Chuo Kikuu lakini kutokana na ukosefu wa fedha wanakosa hiyo fursa muhimu.
Hemed amesema hayo katika mkutano mkuu wa 22 wa Baraza la Masajili la Chuo Kikuu cha Mzumbe uliofanyika katika ukumbi wa Maekani uliopo Kampasi kuu ya Chuo hicho mkoani Morogoro.
Amesema mfuko huo utasaidia wanafunzi wanaongia chuoni na kushindwa kuendelea na masomo yao kutokana na ukosefu wa fedha.
Hemed amesema yenye ni mmoja kati ya waliosoma kwenye chuo kikuu hicho na uanzishwaji wa mfuko utasadifu kauli mbiu ya Chuo kikuu hicho inayosema “ Tujifunze kwa Maendeleo ya Watu”.
Amesema Chuo kikuu hicho ni kati ya Vyuo vikuu nchini kinachofanya vizuri kwa kutoa viongozi wa ngazi ya juu ikiwemo Rais Samia Suluhu Hassan na wengine waliopo serikalini na sekta binafsi.
“ Hata mimi najivunia kuwa zao la Chuo kikuu Mzumbe kwani nilisoma shahada ya umahiri kwenye biashara na uchumi ambayo imenisaidia katika kazi yangu ya mwanzo ya afisa Mnadhimu wa Wizara ya biashara nikiwa Pemba “ amesema Hemed
Hemed pia ameushauri uongozi wa Chuo kikuu hicho kuangalia namna ya kuanzisha mashirikiano na Vyuo vya Zanzibar ili kutanua wigo wa kuchagua Program za kujiufunza na kusogeza fursa ya elimu kwa wazanzibari.
Pia ameutaka uongozi wa Chuo kikuu hicho kuwa sehemu ya kumsaidia Rais Samia na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Hussein Ali Mwinyi katika kutimiza malengo ya kujenga na kuiendeleza Tanzania.