WANAWAKE wilayani Kilosa, Mkoa wa Morogoro wamenufaika na elimu ya sheria ya mirathi, ardhi na ndoa kupitia mpango wa kusaidia jamii katika masuala mbalimbali ya kisheria unaotekekezwa na Kituo cha Msaada wa Kisheria cha Chuo Kikuu Mzumbe.
Mhadhiri wa Sheria wa Chuo Kikuu hicho, Dk Thobias Mnyasenga alisema mjini Kilosa kuwa wataalamu wa sheria kutoka Kituo hicho katika wiki ya kuelekea maadhimishi ya siku ya wanawake Duniani walitembelea wilaya ya Kilosa kuwasikiliza wananchi na kuwapatia elimu ya msaada wa kisheria.
Dk Mnyasenga ambaye ni wakili wa kijitegemea wa mahakama kuu alisema wakiwa wilayani humo kwa muda wa siku tatu walitoa elimu na ushauri wa kisheria kwa wale wasiojiweza katika maeneo mirathi, ndoa na masuala ya ardhi.
Alisema kuwa wananchi wengi waliojitokeza kwa zaidi ya asilimia 92 ni wanawake wakilalamikia masuala ya ardhi na migogoro ya mirathi.
Dk Mnyasenga alisema kwa siku hizo idadi kubwa ya wananchi walijitokeza kutoa malalamiko yao kwenye maneneo mawili kati ya matatu ambayo ni mirathi na ardhi.
“ Wateja waliofika karibu wamegusa maene mawili ,hili la ndoa hatujalipokea, shida kubwa zaidi ni eneo la ardhi wakilalamika kuhusu suala la kupata haki za zao kwenye ardhi kwenye uvamizi wa mashamba wenyewe kwa wenye na suala la uvamizi wa migogoro kati ya wakulima, “ alisema Dk Mnyasenga.
Alisema waligundua ya kwamba wananchi wengi wahajui namna ya kufuata mlolongo wa kisheria ambao ungewawezesha kusaidia kupata haki zao kwa haraka, kwani wamekuwa wakizunguka kwenda kwa mkuu wa wilaya na vituo vya haki za binadamu na maeneo mengine.
“Muda anaoutumia mwingi na baadaye anajikuta yupo nje ya muda ambao angefuata njia za utaratibu wa kisheria za kimahakama angeweza kupata haki yake bila kupoteza muda zaidi” alisema Dk Mnyasenga.
Dk Mnyasenga ameishauri jamii kufuata taratibu za kurithi mali anazoacha marehemu kwa njia ya kisheria kwani kushindwa kufuata sheria kunachangia kukithiri kwa migogoro ya ardhi ambayo chanzo chake kinatokana ukosefu wa kupatikana kwa mirathi ya urithi kisheria.
Kwa upande wake Mhadhiri na Mratibu wa Kituo cha Msaada wa Kisheria Chuo Kikuu Mzumbe, Wakili Bernadetha Iteba ,alisema kituo hicho kinajihusisha na kutoa msaada wa kisheria bure kwa wananchi ambao hawana uwezo wa kumudu gharama za kisheria na kuweza kuwalipa mawakili na watu wa aina hiyo wanapokelewa katika kituo hicho.
“Watu hawa akishafika wanapokelewa na kuatiwa huduma bure ziwe za ushauri ama kwa njia ya elimu au kuandaa nyaraka mbalimbali kwamba huyu mtu sasa anataka kwenda kufungua shauri ya mirathi lakini hajui namna ya kuandaa nyaraka “ alisema wakili Iteba.
Wakili Iteba alisema kituo pia kinatoa msaada wa uwakilishi mahakamani kwa zile kesi ambazo ni nyeti baada ya kuona ya kwamba Mwananchi huyo asipopewa wakili wa kwenda kumsaidia na kumsimamia mahakamani anaweza kupoteza haki basi kituo kinampa wakili bure atakaye enda kusaidia na kumsimamia.
Alisema kuazishwa kwa kituo hicho ni moja ya njia ya kuiunga mkono serikali kwa maana ya mhimili wa mahakama kwa sababu sheria chini ya katiba yetu inatambua na kutamani ya kwamba wananchi wote wanapokuwa na matatizo ya kesi waweze kupewa haki ya kusikilizwa na kuwakilishwa kwa vizuri zaidi .
Wakili Iteba alisema chuo kikuu hicho kupita kitivo cha sheria kimeweka mkakati wa kuwatembelea wananchi maeneo mbalimbali ndani ya Wilaya ya Mvomero na nyingine za jirani na kutoa elimu na semina kuhusu masuala ya mirathi, ardhi na ndoa .
Katika hatua nyingine wanajumuiya ya wanawake wa chuo kikuu hicho walikabidhi misaada ya vitu mbalimbali vikiwemo vifaa vya shule kwa wanafunzi na waathirika wa mafuriko wilayani Kilosa .