Nabi aita mashabiki kwa Mkapa

KOCHA Mkuu wa Yanga, Nasredeen Nabi amewataka mashabiki wa timu hiyo kujitokeza kwa wingi Uwanja wa Benjamini Mkapa kesho kwenye mchezo wa Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kati ya Yanga na Marumo Gallants ya Afrika Kusini.

Anasema kikosi chake kipo tayari kwa mchezo huo na kwamba wachezaji wake wana ari kubwa na tayari wamefanyia kazi maeneo yenye upungufu. Hata hivyo Nabi ametoa hadhari kwa mashabiki wanaoenda uwanjani wakiwa na matokeo mfukoni.

“Mechi tunayoenda kukutana nayo ni ngumu, kwa sababu Marumo ni timu bora na ndio maana wamefika nusu fainali, wasingekuwa bora basi wasingefika hatua hiyo kubwa, kwa hiyo siyo timu ya kubeza hata kidogo.

Advertisement

“Mara nyingi mashabiki wanaamini kucheza nyumbani ni rahisi kushinda, ila ni lazima wafahamu mchezo huu una mikondo miwili, yaani nyumbani na ugenini, kwa hiyo mbinu nyingi zinatumika kwenye michezo ya aina hii kwenye kila timu,” amesema.

Kocha huyo raia wa Tunisia ameongeza kuwa hana uhakika wa kuipata huduma ya beki wa kulia wa timu hiyo, Djuma Shaaban ambaye anasumbuliwa na mafua, hivyo kushindwa kufanya mazoezi na wenzake.

Kwa upande wake kipa wa timu hiyo Metacha Mnata, amesema wachezaji wa Yanga wanafahamu umuhimu wa mchezo huo na matamanio yao ni kuandika historia ya kucheza fainali ya michuano hiyo ya pili kwa ukubwa ngazi ya klabu Afrika.

Metacha ambaye mpaka sasa ameichezea timu hiyo mchezo mmoja kwenye michuano hiyo, anasema watacheza kwa tahadhari kubwa kutokana na ubora wa wapinzani wao, hasa wakiwa ugenini.

“Sisi wachezaji tunatamani kuwa sehemu ya historia ya klabu yetu, kila tukikaa tunazungumza jinsi ya kupata matokeo kwenye mchezo wa kesho ili kufuzu fainali.

“Tunafahamu Marumo ni wazuri sana hasa wakiwa ugenini, lakini tumekaa na kuangalia video zao kwa hiyo tupo tayari kutekeleza maagizo ya walimu wetu baada ya kumsoma mpinzani wetu.”

Yanga inasaka rekodi ya kucheza fainali ya michuano hiyo kwa mara ya kwanza na wataanzia nyumbani Uwanja wa Benjamini Mkapa kesho kabla ya kurudiana Mei 17, mwaka huu nchini Afrika Kusini.

1 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *